Kilombero kukusanya 38/-bilioni

27Feb 2016
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Kilombero kukusanya 38/-bilioni

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilombero, Morogoro inakadiria kukusanya Sh. 38,093,031,411 kutoka vyanzo vyake mbalimbali vya mapato katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Ashiatu Kijaji.

Akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Azimina Mbilinyi, alisema kati ya fedha hizo zitatumika kwa ajili ya shughuli ya miradi ya maendeleo.

Alifafanua kuwa katika miradi ya maendeleo halmashauri imetenga Sh. 2,054,640,000 kwa ajili ya utekelezaji wake katika kipindi hicho.

Aidha, alisema katika ruzuku hiyo ya miradi ya maendeleo imetenga Sh. 1,027,320,000 kwa kuzingatia mfumo wa upelekaji wa rasilimali katika ngazi za chini za serikali za mitaa.

Alisema miradi itakayotekelezwa ni ile iliyopo katika sekta za kilimo, maji, afya, ujenzi na elimu.

Akizungumzia bajeti ya mwaka uliopita ya 2015/2016, alisema halmashauri hiyo iliidhinishiwa Sh. 47,143,844,253 kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali na hadi kufikia Desemba 2015, halmashauri imepokea Sh. 20,979,220,721, sawa na asilimia 44.59 ya makadirio ya mwaka 2015/2016.

Alisema kati ya fedha zote zilizopokelewa makusanyo ya ndani hadi kufikia Desemba 2015, halmashauri ilikusanya Sh. 2,850,066,196.69 sawa na asilimia 45.72 ya makisio ya mapato ya ndani ya Sh. 6,233,615,773.

Hata hivyo, alisema utekelezaji wa shughuli ulikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo kuchelewa kwa fedha toka serikali kuu, kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi na mafuta, mwitikio mdogo wa wananchi kuchangia hasa miradi ambayo inahitajika, michango ya fedha kutoka kwa wananchi na wakandarasi wengi kukosa uwezo wa kifedha kukamilisha miradi kwa wakati.

Alisema ili kukabiliana na changamoto hizo za mwaka 2015/2016 halmashauri imejiwekea mikakati mbalimbali kwa mwaka 2016/2017 ikiwamo kuendelea kuhamasisha wananchi kuchangia miradi ya maendeleo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe, alisema kila kiongozi katika eneo lake lazima atimize wajibu wake na yeye atakuwa tayari kutumbua majipu kabla hajatumbuliwa yeye.

Habari Kubwa