Kiwanda cha mionzi dawa kuanza Juni

10May 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kiwanda cha mionzi dawa kuanza Juni

SERIKALI imeliambia Bunge kuwa kiwanda cha kutengeneza mionzi dawa kinatarajiwa kuanza kufanya kazi Juni mwaka huu.

Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel, alibainisha hayo bungeni jana alipokuwa akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Mtambwe, Khalifa Mohamed Issa (ACT-Wazalendo).

Katika maswali yake, mbunge huyo alitaka kujua mkakati wa serikali wa kuangalia namna ya kupunguza gharama za uagizaji wa vifaa tiba kwa ugonjwa wa saratani.

“Pia magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakiongezeka kila wakati lakini asilimia 20 ya fedha zinagharamia magonjwa haya, je, sio wakati muafaka sasa wa serikali kuunda tume ya kushungulikia magonjwa haya kama ilivyo TACAIDS?” Alihoji.

Akijibu mawali hayo, Naibu Waziri Mollel alisema kiwanda hicho kitaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa takribani nchi tano za Afrika kuwa na kiwanda cha aina hiyo.

Hata hivyo, alisema si jambo jema kuanzisha tume ya kushughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kuwa fedha nyingi zitatumika kwa ajili ya utawala badala ya fedha hizo kwenda kuwahudumia watu.

Alisema kinachopaswa ni kutoa elimu na kuimarisha utoaji wa huduma za afya.

Katika swali la msingi, mbunge huyo alihoji mikakati ya serikali katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.

Mollel alisema kuwa mkakati wa serikali katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ni kutoa elimu kinga, kusomesha madaktari bobezi kwenye eneo hilo pamoja na ununuzi wa dawa na vifaa tiba vya teknolojia ya juu katika utambuzi na tiba ya magonjwa yasiyoambukiza.

Habari Kubwa