Kiwanda cha saruji chafungiwa kwa uchafuzi wa mazingira

19Mar 2016
Lulu George
Tanga
Nipashe
Kiwanda cha saruji chafungiwa kwa uchafuzi wa mazingira

SERIKALI imekifungia kiwanda cha kutengeneza saruji na chokaa cha Rhino, jijini Tanga kutokana na uchafunzi wa mazingira.

Luhaga Mpina.

Aidha, serikali imetoa siku 90 kwa Kiwanda cha Maziwa cha Tanga Fresh, kurekebisha mfumo wa maji taka.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira na Muungano, Luhaga Mpina, alitoa uamuzi huo jana baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja kwenye viwanda hivyo.

Mpina alisema serikali haitavumilia uchafuzi wa mazingira ambao kwa kiasi kikubwa unaleta athari na kutishia hali ya usalama wa maisha ya wananchi wake.

Kadhalika aliwaagiza wataalamu wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa ili waweze kuyakamilisha kwa wakati.

“Hali ya uchafuzi wa mazingira inaofanywa na hivi viwandani, nimeuona mwenyewe haiwezekani wewe Tanga Fresh utiritishe maji machafu kwenye makazi ya wananchi halafu huyu naye vumbi lote linawarudia wananchi, hivi kweli ni kusudi au ni nini kwani sheria mnazijua na NEMC naamini walishawapa mwongozo, sasa nawafungia mpaka hapo mtakapokaguliwa tena na kuonekana mmejirekebisha,” alisema.

Akizungumzia hali hiyo, mwakilishi wa wananchi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Maweni, Joseph Calvas, alisema kumekuwa na vumbi zito linalitoka katika kiwanda hicho ambalo kwa kiasi kikubwa linawaathiri wanafunzi wa Shule ya Sekondari Donbosco, jirani na kiwanda hicho.

“Mheshimiwa waziri hivi viwanda kwa ujumla ni changamoto kubwa sana kwa wakazi wa kata yangu ukipita barabara hii ya Kange pale Tanga Fresha, harufu inayotoka utashangaa kwani mfereji wao wa maji taka unapita barabarani, lakini na hawa nao Rhino, wamezima mitambo leo bila shaka walijua unakuja, lakini ingewezekana kwa vumbi ,” alisema Calvas.

Ofisa Afya wa Jiji la Tanga, Kizito Nkwabi, alisema walishatoa onyo kwa kiwanda cha Rhino kutokana na hali hiyo ya uchafuzi wa mazingira.

Naye Mkaguzi kutoka NEMC, Novatus Mushi, alisema kiwanda cha Rhino kilishawahi kutozwa faini Sh. milioni 17 kwa kosa la kuchelewa kulipa kodi ya mazingira kutokana na uzalishaji wa chokaa.

Habari Kubwa