Kiwanda chajengwa kuongeza thamani mazao ya viungo

26Nov 2021
Hamida Kamchalla
Muheza
Nipashe
Kiwanda chajengwa kuongeza thamani mazao ya viungo

ASILIMIA 80 ya mazao ya viungo yaliyokuwa yakiuzwa na kusafirishwa bila kuongezwa mnyororo wa thamani katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, yameanza kuongezwa thamani baada ya uwekezaji mkubwa wa Kiwanda cha kuchakata mazao hayo cha Trianon Spicies.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Edward Rukaka, alimweleza jana Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratus Ndejembi, kuwa wilaya hiyo ndio inayoongoza kwa kilimo cha mazao hayo.

"Mazao haya ni ya msimu na Wilaya ya Muheza ndiyo inayoongoza kwa mikoa ya Tanzania Bara kulima mazao ya viungo.

"Sisi ndiyo tunaoongoza takribani asilimia 80 ya mazao yote, kwa sababu kiwanda chetu kinachakata, kusafisha na kusafirisha mazao haya nchi za Ulaya kwa wingi.

"Kwa mwaka jana wote uzalishaji ulikuwa tani 200, na sisi tunasafirisha tani 120. Kwa hiyo utaweza kuona sisi tuna soko kubwa sana na kwasababu tunafanya kazi zaidi na wakulima kama 1200 kwa hiyo sehemu kubwa ya mazao yao kupitia AMCOS na hata wakulima mmoja mmoja, yote yanakuja hapa," alisema.

Rukaka alibaisha kwamba kwa upande wa masoko, hali ni nzuri baada ya wao kununua mazao ya wakulima wanawalipa fedha zao na wao kuanza uchakataji na kufungasha lakini pia kusafirisha nchi za Ulaya.

"Soko kubwa zaidi liko Ulaya ingawa yakifika kule na wao wanasafirisha nchi nyingine kwa sababu wale ndio wana masoko makubwa kwa muda mrefu.

"Tuna wateja wetu hawa wanaotoka nchi nne, ambazo mahitaji yao yalikuwa makubwa katika kipindi hiki cha Uviko-19, tumejitahidi sana kupeleka mzigo mkubwa na tumepata manufaa kama kiwanda.

"Toka tumewekeza kiwanda mpaka sasa tumekusanya jumla ya mazao yenye thamani ya Sh. bilioni 1.2.

"Lakini pia kwenye mafanikio siku zote hapakosi changamoto, miundombinu ya barabara kipindi cha mvua, barabara ni tatizo sana na bahati mbaya au mzuri maeneo yote wanayolima mazao haya yako milimani. Kwa hiyo usafiri wake unakuwa ni pikipiki, serikali inajitahidi kutengeneza barabara lakini tungeomba barabara hizo zingefika hata katika maeneo yale," alisema.

Naibu Waziri Ndejembi alisema: "Serikali imejipanga katika kuongeza thamani mazao ya thamani, sasa wenzetu hawa wamejikita zaidi katika mazao ya viungo ambayo yana thamani kubwa hasa kwenye soko la nje, sasa wakulima wetu hawa wadogo wadogo wataweza kulima mazao ya viungo.

"Mimi naliangalia hii kwa mrengo wa TASAF kwa zile kaya masikini kwamba mtu wa kaya masikini akiwa na 'kashamba kake kadogo', ina thamani na soko lake pia lipo kwenye kiwanda hiki, akauza zao likaongezwa thamani na kupelekwa nje, tayari tunaweza kunyanyua hawa watu wa kaya masikini kunyanyua kipato chao, inawasaidia kuwa na kitu cha ziada kama, nyumba bora, maisha bora pamoja na kuwapeleka watoto wao shule."

Ndejembi pia alitoa pongezi kwa wenye kiwanda hicho na kusisitiza elimu zaidi itolewe kwa wananchi kulima mazao hayo ambayo wengi hawana uelewa au mwamko wa kilimo hicho.

Naibu Waziri alikuwa mkoani Tanga kwa ziara ya siku tatu iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Habari Kubwa