Kiwango ukuaji mikopo sekta binafsi chapaa

23Jun 2022
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Kiwango ukuaji mikopo sekta binafsi chapaa

WIZARA ya Fedha na Mipango imesema kiwango cha ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kimeongezeka kufikia wastani wa asilimia 8.4 katika kipindi cha Julai 2021 hadi Aprili 2022.

Naibu Waziri Hamad Hassan Chande, alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tumbatu (CCM), Juma Othman Hija.

Mbunge huyo alihoji kwa kiasi gani lengo la Benki Kuu la kutoa mikopo kwa sekta binafsi ili kutoa fursa za ajira hususan kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati limefikiwa.

Chande alijibu, kiwango hicho kimeongezeka ikilinganishwa na wastani wa asilimia 4.3 katika kipindi cha Julai 2020 hadi Aprili 2021.

Aidha, alisema kuanzia Desemba 2021, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulikuwa zaidi ya asilimia 10 na Aprili 2022, ukuaji huo ulifikia asilimia 13.4.

Awali, alifafanua kuwa Sera ya Fedha ya Mwaka 2021/22 imeainisha shabaha ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi wa asilimia 10.6 ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa gharama nafuu na kuongeza ukwasi katika uchumi.

Pia alisema kutokana na utekelezaji wa sera hiyo, kiwango cha ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kimeendelea kuongezeka.

Hata hivyo, alisema kutokana na mwenendo huo, matarajio ni kwamba lengo la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi la asilimia 10.6 kwa mwaka 2021/22 litafikiwa na hivyo kuchangia uwekezaji, uzalishaji na kuongeza ajira nchini.