Kodi majengo yagota bil. 37/-

03Sep 2017
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
Kodi majengo yagota bil. 37/-

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imekusanya Sh. bilioni 37.1 kutokana na kodi ya majengo kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, malengo kwa ajili ya makusanyo ya kodi ya mwaka huo wa fedha yalikuwa ni kukusanya Sh. bilioni 58. Dk. Mpango alieleza hayo Julai 15, mwaka huu, hivyo kimahesabu, kiasi kilichokusanywa si haba kwa kuanzia, ambacho ni sawa na asilimia 63 ya malengo.

Ukusanyaji wa kodi hiyo umefanyika kwa miezi mitatu baada ya TRA kutoa muda wa mwisho wa kulipa na kutangaza adhabu kwa watakaoshindwa kutimiza wajibu huo wa kisheria.

Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015, anayebainika kutolipa kodi hiyo hulipa faini ya kati ya Sh. 200,000 hadi milioni moja, au kifungo.

Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo, alisema fedha hizo zimekusanywa kutoka majiji, miji na manispaa 33 nchini.

Alisema makusanyo hayo kwa mwaka wa fedha 2015/16 yalikuwa ni Sh. bilioni 28.2.

 “Kukusanya kodi kumetokana na maamuzi kuhakikisha zinakusanywa mahali pamoja na kuondoa kero ya kulipa sehemu tofauti. Sheria imeturuhusu kukusanya kodi maeneo yote isipokuwa vijijini,” alisema.

Aliongeza kuwa katika ukusanyaji huo, wazee wa kuanzia miaka 60 ambao wamestaafu wanaweza kuomba msamaha wa kodi hiyo kutoka ofisi ya TRA ya eneo husika.

Alisema pia majengo ya ibada na serikali yanayohudumia wananchi, makazi ya rais na viongozi wa serikali, hospitali na shule za umma, maktaba za umma na makaburi, vyote vimesamehewa.

“Ili kuwezesha mpango wa kukusanya kodi za majengo, waliothaminishwa wataendelea kulipa asilimia 0.15 ya thamani ya jingo. Ambao bado watalipa Sh. 10,000 kwa nyumba za kawaida na ghorofa 50,000,” alisema.

Kwa mujibu wa Kayombo, makusanyo yanaendelea na sasa ni mwaka mpya wa fedha wa 2017/18, hivyo moyo na ari ya ulipaji inapaswa kuendelea ili kupata fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema katika ukusanyaji huo, kodi haikusanywi kwenye nyumba za nyasi, miti au zisizo za kudumu.

Kayombo alibainisha changamoto zilizopo kuwa ni kuibuka kwa matapeli, hasa jijini Dar es Salaam, ambao walidai fedha za fomu kwa wananchi kati ya Sh. 10,000 hadi 100,000, na kuwaonya kuacha kufanya hivyo kwa kuwa fomu zinatolewa bure na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.

Alibainisha changamoto nyingine kuwa ni kuwapo kwa watu wengi wanaotaka kulipia, pamoja na idadi kubwa ya majengo ambayo hayajaingizwa kwenye mfumo wa walipa kodi.

Aidha, alisema TRA imerahisisha ulipaji wa kodi hiyo na nyingine, kwa kusogeza ofisi karibu na walipakodi, huku akitolea mfano wa jiji la Mwanza ambako wamefungua ofisi mpya katika maeneo ya Buzuruga na Nyegezi.

 Aidha, alisema wamejenga ofisi katika mikoa mipya ya Songwe, Geita, Simiyu, Katavi na Njombe, na kwamba wanaendelea kutafuta maeneo mapya ya kuweka ofisi kwa jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano na kurahisisha ulipaji.

Habari Kubwa