Kodi ya pango mabanda kituo cha mabasi Dodoma yapaa

09Aug 2016
Peter Mkwavila
Dodoma
Nipashe
Kodi ya pango mabanda kituo cha mabasi Dodoma yapaa

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma, imepandisha kodi ya pango kwenye mabanda ya wafanyabiashara wa kituo cha mabasi ya daladala na yaendayo mikoani kutoka Sh. 10,000 hadi 100,000 kwa mwezi.

kituo cha mabasi dodoma.

Kwa mujibu wa barua ambayo Nipashe iliiona yenye kumbukumbu namba HMD/F.20/16/63 iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi, Clemence Mkusa, kwenda kwa Umoja wa Wafanyabiashara wa kituo cha mabasi ya daladala ya Jamatini, kwa sasa kodi ya pango ya kufanyia biashara kwa eneo la mjini ni kati ya Sh. 100,000 na Sh. 300,000.

Barua hiyo ilisema sababu ya kupandisha bei ni eneo ambalo lina wateja na liko katikati ya mji.

Ilifafanua kuwa maeneo ya katikati ya mji yana mzunguko mkubwa wa biashara kutokana na wingi wa watu hivyo kiasi cha pango cha maeneo hayo hakipaswi kuwa sawa na kile cha nje ya mji ambacho ni Sh. 10,000.

“Kutokana na mabadiliko ya hali ya kiuchumi na mfumko wa bei uliopo sasa, kiasi cha kodi ya pango kinachokusanywa na Manispaa kutokana na wapangaji wake kwa Sh. 10,000, hakina thamani sawa na wakati ule ambao kilipangwa kwa kuwa ni muda mrefu na thamani ya fedha imeshuka,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Hata hivyo, ilifafanua kuwa Manispaa ina maeneo mengine ya kufanyia biashara katika masoko yaliyopo pembezoni ambayo yana nafasi ya wazi na wale watakaoshindwa kulipa kodi kwa viwango vipya waombe nafasi katika masoko mengine na kuendelea na biashara zao.

Wakizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha wafanyabiashara wa kituo hicho cha daladala, walisema awali walikuwa wakilipa Sh. 10,000, lakini Manispaa imetoa barua ya mabadiliko ya viwango vya pango na sasa wanatakiwa kulipa Sh. 100,000.

Hata hivyo, Katibu wa Umoja wa Wafanyabiashara Jamatin, Sakina Issa, alisema kiwango hicho cha Sh. 100,000 ni kikubwa na hawana uwezo wa kulipa na wapo tayari kufunga mabanda yao.

Alisema wakati Manispaa ikitaka kupandisha kodi, haikuwashirikisha wafanyabiashara kupata mawazo kutoka kwao.

“Fikiria mama lishe anauza biashara yake hapo hata Sh. 10,000 ni kubwa kwake, Manispaa ielewe kwamba sisi tuko tayari kulipa kodi ya pango Sh. 20,000 hadi Sh. 25,000, lakini laki moja hatuwezi,” alisisitiza Katibu huyo.

Naye Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Neema Ally, alisema amesikitishwa na hatua hiyo na kwamba serikali imeonyesha dharau kwa kuwataka kufanya biashara kwenye maeneo ambayo yatalingana na kodi wanayoitaka.

“Serikali imetumia lugha ya kuudhi kwa kuwa tunalipa kodi ya pango Sh. 10,000, wanatutaka tukafanye biashara sehemu yenye hadhi ya Sh. 10,000 eti kama tutashindwa kulipa laki moja, inauma sana yaani wanataka tu kutupeleka kwenye maeneo ambayo tutaua mitaji yetu,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Melkion Komba, alithibitisha kupanda kwa pango hilo.

Komba alisema manispaa hiyo iko katika mkakati wa kuongeza mapato na wamefanya utafiti wa kutosha na kufikia hatua hiyo.

Habari Kubwa