Kuchezea mizani jela miaka 3

27Jun 2016
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Kuchezea mizani jela miaka 3

WANUNUZI wa pamba watakaobainika wanachezea mizani kwa lengo la kuwaibia wakulima wa zao hilo, watapewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela bila kuwapo na faini, Kaimu meneja Wakala wa Vipimo mkoani Shinyanga, Maneno Mwakibete, alitoa tahadhari hiyo juzi.

Mwakibete alitoa tahadhari hiyo kutokana na kukithiri kwa tabia hiyo miongoni mwa wanunuzi mawakala ambao si waaminifu.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa pamba mkoani hapa, Mwakibete alisema msimun huu, Wakala wa Vipimo umedhamiria kuhakikisha mkulima ananufaika na kilimo hicho kwa kuwakamata mawakala "wajanja" wa kuchezea mizani na kuwafunga jela.

“Msimu huu, wakala atakayekamatwa akichezea mizani kwa lengo la kumuibia mkulima, hakutakuwa na utozwaji faini kama ilivyozoeleka," alisema Mwakibete, "bali moja kwa moja atafikishwa mahakamani na kutolewa hukumu ya kwenda jela miaka mitatu.”

Naye Ofisa Kilimo wa Mkoa, Dotto Maligisa alisema kuna uwezekano zao la pamba likatoweka ndani ya miaka mitatu ijayo, kutokana na wakulima kukabiliwa na changamoto lukuki, hivyo kukata tamaa ya kulilima.

Maligisa alisema msimu huu, mkoa ulitaraji kulima hekta 106,409 lakini kutokana na wananchi kususa, zimelimwa hekta 48,009 hali ambayo inahatarisha mkoa kushuka kiuchumi.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, John Mongella aliwaagiza wakuu wa wilaya zote tatu mkoani humo kutengeneza kikosi kazi kinachohusisha polisi na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), kuwakamata mawakala wanaochezea mizani ya pamba na wale wanaochafua zao hilo.

Habari Kubwa