Kudorora bei ya mchele kwaathiri kilimo

18Jan 2021
Grace Mwakalinga
Mbarali
Nipashe
Kudorora bei ya mchele kwaathiri kilimo

KUDORORA kwa bei ya bidhaa ya mchele kumeleta athari kwa baadhi ya wakulima wilayani Mbarali na kusababisha kukosa fedha za kuandaa mashamba ya mpunga msimu huu wa kilimo.

Wakizungumza juzi na wilayani humo, baadhi ya wakulima walisema miaka ya nyuma msimu kama huu mchele huuzwa kati ya Sh. 1,800 hadi 2,000 kwa kilo moja, lakini kwa sasa bei yasokoni ni kati ya Sh. 1100 na 1,500.

Wille Mwakasoke, mkulima kutoka Igurusi wilayani humo ambaye pia ni mjasiriamali, alisema gharama za uzalishaji wa zao hilo ni kubwa ikilinganishwa na bei ya soko, hali inayowapa wakati mgumu wakulima kumudu gharama hizo.

Alisema kuyumba kwa bei ya mchele kuna athiri baadhi ya shughuli nyingine za kiuchumi zikiwamo biashara ndogo ambazo hutegemea mzunguko wa fedha unaotokana na biashara hiyo.

“Mwezi kama huu na kuendelea wakulima huwa wanauza kilo 20 za mchele kati ya Sh. 36,000 na 40,000, tofauti na mwaka huu ambapo bei iko chini sana na soko liliyumba tangu mwaka jana wakati changamoto za kipindi cha corona,” alisema Mwakasoke.

Huruma Mwakanyamale, muuza nafaka ikiwamo mchele, alisema licha ya bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei ya chini, lakini hata kasi ya utokaji ni ndogo ikilinganishwa na kipindi cha nyuma kabla ya janga la corona.

“Ingawa tumeanza kujijenga upya kibiashara baada ya kipindi cha mpito cha corona kati ya mwezi Machi na Mei 2020, jitihada zetu hazifikiwi haraka kutokana ukosefu wa soko la uhakika hasa kwa mchele ambao ni zao kuu kwa Wilaya ya Mbarali,” alisema Mwakanyamale.   

Emmanuel Mtaki, miongoni mwa vijana ambao mwaka huu hawezi kujihusisha na shughuli za kilimo baada ya kukosa mtaji, alisema kuwa pamoja na familia yake wameamua kujaribu shughuli ya kuuza chips ili kuendesha maisha yao.

“Mimi ni mkulima, lakini kwa msimu huu nimekwama kuendeleza shughuli hiyo, kutokea kwa janga corona mwaka jana kuliyumbisha mtaji wangu, sitakuwa na uwezo wa kumudu gharama za kilimo hasa kama kukodi shamba, kununua pembejeo na uwezo wa kupata rasilimali watu” alisema Mtaki...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa