Lindi yatajwa kinara kwa bandari bubu

03Dec 2018
Said Hamdani
Lindi
Nipashe
Lindi yatajwa kinara kwa bandari bubu

UWAPO wa idadi kubwa ya bandari bubu katika Mkoa wa Lindi, umetajwa kuchangia upotevu wa mapato ya serikali.

Mkoa huo unatajwa kuwa na bandari bubu zisizopungua 32, huku Wilaya ya Lindi ikiongoza kwa kuwa na bandari za aina hiyo zipatazo 17.

Hayo yalibainishwa na Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mkoa wa Mtwara, Abdirahi Salum, wakati wa kikao kazi na wadau kilichofanyika Manispaa ya Lindi.

Salumu aliitaja Wilaya ya Lindi ndiyo inayoongoza kwa kuwa na bandari bubu (17), ikifuatiwa na Kilwa yenye bandari bubu 15 na kuzitaja kuwa ni Ruvu, Kijiweni, Mchinga moja na mbili, Shuka, Rushungi, Msangamia, Ngongo, Sudi Bay, Mmongomongo, Mingoyo, Jange, Kela, Ras Ruvula na Ras Chani.

Zingine ni M’buyuni, Mtandango Kilutu, Matapatapa, Msimwale, Mtoni, Mgongeni, Mayungiyungi, Kela, Milamba, Kilwa Kivinje, Pande, Lihimalyao, Mapimbi 1 na 2, Nakimwera, Kisongo, Kilamba, Masoko Pwani, Kilamba, Sangalungu, Sanje ya Kati na Sanje Majoma.

Alisema kuwapo kwa bandari hizo na zingine zisizo rasmi kuna athari kubwa, ikiwamo za kiuchumi, kisiasa na mambo yote mabaya hujificha katika bandari bubu, hivyo upo umuhimu wa kuzitambua na kuzifanyia maamuzi ya kuzirasimisha zile zitakazowezekana.

“Bandari ni moja ya kiungo muhimu cha biashara, pia lango kuu la biashara ya kitaifa na kimataifa, hivyo uwapo wake upo kisheria ya Bunge namba 17/2004,” alisema Salum.

Kaimu Meneja huyo alisema katika kila bandari kuu, zipo bandari ndogo zinazotambulika kisheria na kuzitaja kuwa ni Kisiju, Bagamoyo na Mafia zilizoko chini ya Bandari ya Dar es Salaam.

Zingine ni Pangani (Bandari ya Tanga) na Kilwa Masoko na Lindi Mjini zilizoko chini ya Bandari ya Mtwara.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaibu Ndemanga, alisema uwapo wa wingi wa bandari bubu kunahatarisha usalama wa nchi, kwa sababu utawapa mwanya watu wasiolitakia mema taifa letu kuingia wakati wowote kupitia njia hizo.

 

Habari Kubwa