Maadhimisho ya ushirika leo

09Oct 2019
Godfrey Mushi
Moshi
Nipashe
Maadhimisho ya ushirika leo

MAADHIMISHO ya Siku ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo nchini (Saccos) yanafanyika leo jijini Arusha.

Kaimu Mrajis Mkuu wa Vyama vya Ushirika, Tito Haule ndiye atakayefungua maadhimisho hayo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT Ltd-1992), Dk. Gervas Machimu.

Kwa mujibu wa Dk. Machimu, awali mkutano huo ulikuwa ufunguliwe jana, lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao, Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Tito Haule, amethibitisha atafungua mkutano huo leo.

Vyama hivyo pamoja na mambo mengine vitatafakari na kushirikishana namna bora ya kufanikisha adhima ya utoaji wa huduma rafiki na jumuishi za kifedha kwa Watanzania.

Alisema zaidi ya vyama 200 vya ushirika wa akiba na mikopo nchini, vimejiandikisha kushiriki ili kupata uzoefu wa kubadilisha maisha ya watu na kufanikisha ndoto za wananchi na hasa wenye kipato cha chini ndani ya jamii ya Watanzania.

“Kwa sababu nia yao ni kuwainua kiuchumi, vinataka kuwahakikishia Watanzania kipato endelevu kitakachowawezesha kumudu gharama za maisha,” alieleza.

Aidha, alisema maadhimisho hayo kwa Tanzania yametangulia kufanyika ili kutoa fursa kwa Saccos za Tanzania kuungana na Saccos nyingine za Afrika katika maadhimisho yatakayofanyika Mombasa, Kenya.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni iliyotolewa na Baraza la Vyama vya Akiba na Mikopo Ulimwenguni ni ‘huduma kwa kijamii, kuufikia ulimwengu’.

Habari Kubwa