Mabadiliko tabia nchi yashusha uzalishaji zabibu

29Sep 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mabadiliko tabia nchi yashusha uzalishaji zabibu

MABADILIKO ya tabia nchi yaliyochangia kuongezeka kwa mvua Mkoa wa Dodoma mwaka 2020 ni miongoni mwa sababu za kupungua kwa uzalishaji wa zabibu msimu huu.

Nipashe mwishoni mwa wiki ilitembelea maeneo maarufu na yenye mashamba makubwa ya zabibu katika kata ya Mpunguzi, Mbabala na Hombolo na kubaini kuwapo na uzalishaji mdogo ikilinganishwa na misimu iliyopita.

Wakizungumza hali hiyo, wakulima hao walisema kwa mwaka huu uzalishaji sio mzuri kwa kuwa zimeadimika kabla ya msimu kuisha.

“Mwaka huu mavuno yalikuwa kidogo kutokana na mvua kunyesha sana, yaani kwa kiwango kikubwa miche iliishia kupata maua bila kuzaa na mingine iligoma kabisa kutoa matunda,” alisema mkulima Maneno Joseph.

Alisema mwaka huu kwao ni hasara kutokana mavuno  kidogo licha ya kuwapo na bei nzuri kwenye soko.

“Unakuta shamba lilikuwa la kuvuna tani tano za zabibu, lakini amevuna kilo 600, au shamba lingine kama mkulima alichelewa kuliandaa basi hajapata kapiga,” alisema.

Kadhalika, Nipashe ilizungumza na wachuuzi wa zabibu ambao nao walieleza kilio chao kuwa kwa sasa zabibu hazipatikani kwa urahisi na huweka oda siku mbili au tatu ndio wape mzigo tofauti na ilivyokuwa awali kila siku kupata mzigo.

Mmoja wa wachuuzi, Zawadi Manzije, alisema biashara imekuwa ngumu kwao kutokana kuuziwa kwa gharama kubwa.

“Wateja wanajua zabibu zinalimwa hapa na ni bei rahisi, hivyo akikuta anauziwa kichane kimoja kwa Sh.1,000 au 2,000 analalamika maana amezoea kununua ile ya Sh. 1,000 kwa Sh.300 hadi 500,” alisema.

Kwa upande wake, mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza mvinyo cha Alko Vintages, Archard Kato, alisema mahitaji ya zabibu yamekuwa makubwa licha ya wakulima kuongeza zaidi uzalishaji.

“Kutokana na hali hii wameathirika wakulima kutokana na mazao yao kupungua na hata sisi wasindikaji pia tumeathiriwa na hali hii,” alisema.

Akizungumzia hali hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, alikiri kuwa uzalishaji wa zabibu msimu huu umeshuka huku akitaja sababu kuu mbili kuwa ni mvua kubwa na kuyumba kwa soko la dunia kutokana na uwapo wa ugonjwa wa corona.

“Ni wazi kabisa katika maeneo mengi nchini mvua zilikuwa nyingi na zimefika kwenye maeneo ambayo zabibu inalimwa ikiwamo Mkoa wa Dodoma, sasa ilipotokea na ilisababisha baadhi ya mazao kuoza, zabibu ikifikia hatua ya kuiva na ikapata mvua kubwa mara nyingi zinaoza, uzalishaji tutarajie kushuka zaidi,” alisema.

Alisema kwa msimu uliopita uzalishaji wa zao hilo uliongezeka na kufikia tani 15,000 ikilinganishwa na mwaka 2015/16  tani 8,336.

Alitaja mikakati ya wizara kuhakikisha uzalishaji unakuwa mkubwa ni pamoja na serikali kukijengea uwezo Kituo cha Utafiti cha Makutupora kwa ajili ya uzalishaji wa miche ya zabibu kinachotakiwa kuzalisha miche kutoka 100,000 hadi 300,000.

“Kituo kimepewa fedha na wizara na pia kimenunuliwa trekta jipya kwa ajili ya kutanua uzalishaji na kuwa na mashamba mengi ya miche ambayo itachukuliwa na wakulima,” alisema.

 

Kadhalika, alisema wizara imeunda kikosi kazi cha wataalamu kufuatilia mwenendo wa zao hilo ili kutoa mapendekezo yao na kufanyiwa kazi.

“Wizara imeingia makubaliano na kampuni ya bia nchini TBL kutakuwa na vijiji 10 ambavyo vitaanzisha mashamba ya mfano na kufadhiliwa na kampuni hiyo, na tuna hakika kila kijiji kitakuwa na wakulima watatu, tuna imani itakuwa ni nafasi nzuri kwa wakulima kujifunza,” alisema.

Habari Kubwa