Mabati 28,000 yasiyo na ubora yateketezwa

09Aug 2016
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Mabati 28,000 yasiyo na ubora yateketezwa

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limeteketeza mabati 28,000 yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 308 yalioingizwa nchini kutoka China, kutokana na kubainika kuwa hayana viwango na ubora unaotakiwa.

Akizungumza mwishoni mwa wiki baada ya kuteketeza mabati hayo eneo la Kunduchi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Ofisa Mkaguzi wa Ubora wa Huduma na Bidhaa wa TBS, Yona Afrika, alisema mabati hayo hayafai yapo chini ya kiwango kwa kujengea kwa kuwa yanashika kutu mapema.

Afrika alisema kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kupimwa kwa sampuli ya mabati hayo hapa nchini na kubainika kuwa hayajakidhi viwango licha ya kuwa na nyaraka zinazothibisha kukaguliwa na wakala aliyekuwa nchini China.

“TBS walibaini mabati hayo hayana ubora unaotakiwa baada ya kupima sampuli katika maabara ya shirika hilo ambapo walibaini yanakosa vigezo mbalimbali vinavyoyafanya yasipate kutu kwa haraka na kuoza,” alisema Afrika.

Alifafanua kuwa mabati hayo yalikamatwa Bandari ya Dar es Salaam mwaka jana kabla ya kuingizwa sokoni.

“Tuliyachukua na kwenda kuyapima na tukabaini kuwa yako chini ya viwango vinavyotakiwa na hayafai kwa ajili ya kujengea,” alisema.

Alisema mzigo mzima ulioingizwa bandarini hapo ulikuwa na mabati 28,000 ambayo kila moja huuzwa Sh. 11,000, hivyo kufanya jumla ya thamani yake kuwa Sh. milioni 308.

Alisema mabati hayo yaliingizwa hapa nchini na Kampuni ya Kwema Trust, hivyo baada ya kuchukua sampuli na kupima yamebainika yako chini ya kiwango hivyo hayafai kwa kuezekea nyumba bali kwa ajili ya uzio.

Aliwataka Watanzania kuwa makini wakati wa kununua bidhaa ili kuhakikisha zina ubora wa viwango vinavyotakiwa.