Machinga sasa marufuku pembezoni mwa majengo

04Jun 2020
Peter Mkwavila
Dodoma
Nipashe
Machinga sasa marufuku pembezoni mwa majengo

OFISA Masoko wa Jiji la Dodoma, James Yuna, amewataka wafanyabiashara ndogo (machinga) waliovamia pembezoni mwa majengo ya ofisi na yale yasiyoruhusiwa kufanya biashara, kuondoka kwa maeneo hayo kwa kuwa wanakiuka sheria na kanuni ya Halmashauri ya Jiji.

Yuna alisema hayo jana alipozungumza na viongozi wa wafanyabiashara hao jijini Dodoma, kutokana na baadhi yao kufanya biashara pembezoni mwa majengo ya ofisi kinyume cha kanuni na sheria ya jiji.

Alisema kuna wamachinga wanafanya biashara kwenye maeneo ya pembezoni mwa majengo ya ofisi na kusababisha wafanyakazi wake kutokuwa na utulivu na umakini wa kufanya kazi kutokana na kubugudhiwa. 

"Kuna baadhi ya wafanyabiashara wameweka vibanda vya biashara pembezoni mwa majengo ya ofisi mbalimbali ndani ya jiji, hali ambayo imekuwa ikileta usumbufu katika kufanya kazi kwa wafanyakazi wenyewe, hivyo ni lazima wapishe ili wafanye kwa uhuru na usikivu na sivyo vinginevyo," alisema.

Aliwataka viongozi hao wa machinga kuwa mabalozi kwa wenzao ambao wamekuwa wakikiuka sheria kwa kuvamia maeneo kama hayo ya majengo ya ofisi, akiwataka wahakikishe wanatoa elimu, ili waepuke kufanya biashara sehemu zisizoruhusiwa na jiji.

"Uwapo wenu wa viongozi wa machinga ndiyo silaha yangu katika utendaji wa kazi huko mitaani mnakofanya shughuli zenu za biashara, na ndiyo maana hivi sasa hakuna makelele wala migogoro kati yenu na sisi Halmashauri ya Jiji," alisema.

Awali, wakizungumza mbele ya ofisa masoko huyo, viongozi hao walisema kuwa watakuwa tayari kuhakikisha maeneo yasiyo rasmi hayavamiwi ikiwamo kwenye majengo ya ofisi, ili kuondoa usumbufu.

Mwenyekiti wa Machinga Complex 77, Edward Ndahani, amewashauri viongozi wenzake kuisaidia Halmashauri ya Jiji kuondoa mabanda yaliyokaa kwa muda mrefu pasi na kutumika kwa biashara kwa kuwa yanaongeza uchafu jijini.

“Kwenye maeneo yetu tunayosimamia, kuna mabanda ambayo hayafanyi kazi yoyote na yanaonekana ni uchafu, hivyo ninawasihi viongozi wezangu tushirikiana jiji letu katika kuliweka kwenye usafi kwa kuyaondoa mabanda yote yasiyofanya kazi," alisema.

Mwenyekiti wa Machinga Wilaya ya Dodoma, Baraka Marisho, aliwataka wafanyabiashara kushirikiana na Halmashauri ya Jiji kwa lengo la kuondokana na migogoro isiyo ya lazima ikiwamo ya kuvamia maeneo yasiyoruhusiwa.

Habari Kubwa