Machinga waeleza corona ilivyowaathiri

29Jul 2021
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
Machinga waeleza corona ilivyowaathiri

WAFANYABIASHARA wadogo maarufu wamachinga katika Manispaa ya Morogoro, wamesema wanakumbana na ugumu wa biashara na wengine kuelemewa na mikopo kwa sababu wateja wa bidhaa zao wameanza kupungua tangu kuibuka kwa wimbi la tatu la ugonjwa wa corona (UVIKO-19-).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabiashara hao akiwamo mfanyabiashara wa nguo za mitumba Mustapha Chande, alisema biashara zao huwa zinachangamka msimu huu wa kiangazi kuanzia Juni na kuendelea, lakini mwaka huu imekuwa tofauti, hali ambayo wanaihusisha na kuzuka kwa wimbi la tatu.

“Huwa ninakwenda kwenye magulio yaliyo ndani na nje ya Manispaa kwa ajili ya kuuza nguo za kike na za watoto, hali huwa nzuri katika msimu wa kiangazi, lakini msimu  wa kiangazi wa mwaka huu hali ni tofauti na ilivyokuwa nyuma,” alisema.

Chande alisema amekuwa akifanya biashara kwa mauzo yasiyokuwa na faida kwa sababu ya kuuza mzigo mmoja katika magulio mawili au matatu tofauti na miezi mingine kama hiyo, hivyo kuwa na ugumu katika kurejesha mkopo aliyokopa.
 
Naye muuza madafu Manispaa ya Morogoro, Juma Mpili, alisema biashara yake imekuwa ngumu, kwani awali alikuwa akiuza kati ya 50 mpaka 60 kwa siku, lakini kwa sasa anauza kati ya 15 mpaka 25.

“Biashara imekuwa ngumu, ninazunguka kwa baiskeli nikiwa nimebeba mzigo wa madafu kutwa nzima, lakini naambulia kuuza kidogo mengi yanabaki. Biashara imezorota sana, huenda ni corona,” alisema Mpili.

Kwa upande wa kinababa na mamalishe wa Manispaa ya Morogoro na wauzaji wa mboga na matunda walisema wanakumbwa na changamoto ya ugumu wa biashara kutokana na ugonjwa huo.

Yasinta Salumu, anayefanya shughuli zake kwenye Soko la Kuu la Chifu Kingalu, alisema anakumbana na ugumu wa biashara yake ya chakula, na kwamba kwa sasa anapika kilo tano za mchele na bado zikabaki wakati awali alikuwa anapika mpaka kilo 10 kwa siku na wote ulikuwa unaisha.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Ndogo Mkoa wa Morogoro, Faustine Francis, aliwaasa wafanyabiashara hao kuzingatia elimu wanayopewa mara kwa mara juu ya kuepuka misongamano isiyo ya lazima licha ya kuwa wateja wamepungua kwenye masoko mengi.

Naye Msimamizi wa Miradi wa Shirika la Tanganyika la Kuhudumia Wakimbizi (TCRS) Mkoa wa Morogoro, Rehema Samweli, aliwataka wafanyabiashara hao kuongeza juhudi katika kazi na kukumbuka kujiwekea akiba ambayo wataitumia kipindi biashara zao zitakapokwama kama sasa.

Alisema TCRS itaendelea kuwapa elimu ya kumudu kufanya biashara kwa tija na kupambana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.