Machinjio sasa kuanza uchinjaji wa ng’ombe 100, mbuzi 1,000 kila siku

26Jan 2022
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Machinjio sasa kuanza uchinjaji wa ng’ombe 100, mbuzi 1,000 kila siku

MACHINJIO  ya kisasa ya mifugo ya Nguru Hills Ranch Ltd yenye uwezo wa kuchinja  ng’ombe 100 na mbuzi 1,000 kwa siku yaliyoko wilayani  Mvomero  Mkoa wa Morogoro yanatarajiwa kuanza rasmi Machi  mosi, mwaka huu, hivyo  kuchochea ukuaji wa uchumi na ajira.

Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF ), Fortunatus Magambo, alibainisha hayo kwa wahariri kutoka vyombo vya habari waliofanya ziara ya kutembelea na kujionea maendeleo ya  mradi wa  machinjio ya kisasa.

Alisema mradi huo  wa machinjio hayo unamilikiwa kwa ubia  kati ya Serikali kupitia Mfuko wa PSSSF ,  Eclipse Investiment (LLC) na Kampuni ya Busara Investiment (LLP).

Alisema  mradi huo ulianza mwaka 2018,  lakini ugonjwa wa Covid -19 ulipoanza ulisababisha mashine zilizoagizwa kutoka nje kuchelewa kuletwa  pamoja na wataalamu wake  hadi Julai mwaka jana zilipoletwa na kuanza kufungwa na kwamba  kazi hiyo ipo  kwenye hatua ya mwisho.

Naye  Meneja Uhusiano na Elimu kwa wanachama PSSF, James Mlowe,   alivitaka vyombo  vya habari  kuunganisha jamii, Serikali na wadau wa maendeleo katika utoaji wa taarifa sahihi katika uhamasishaji wa kukuza uchumi na maendeleo ya watu.

Mlowe alisema kuwa mfumo wa PSSF umewekeza katika kiwanda hicho wa asilimia 30,ikiwa ni sehemu ya mkakati wake katika uwekezaji wa miradi mbalimbali hasa katika kipindi hiki ambacho taifa limejiwekeza katika uchumi wa viwanda.

“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuunganisha jamii,serikali na wadau katika kuhabarisha umma hasa wanachama wa PSSF ili watambue uwezekaji unaofanyika na michango yao ipo salama katika uwekezaji wenye tija” alisema Mlowe.

Nae Mhandisi wa Kiwanda cha nyama cha Nguru, Zuberi Makazini, alisema mabwawa ya kutibu maji taka kiwandani hapo malighafi zake zinazotumika ni za kisasa na hukithi vigezo vya kimataifa.

Habari Kubwa