Machinjio yatakiwa kujenga kiwanda cha kuchakata ngozi

07Nov 2016
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Machinjio yatakiwa kujenga kiwanda cha kuchakata ngozi

MACHINJIO ya mifugo ya Arusha Meat yaliyopo Sakina jijini hapa yametakiwa kuanzisha kiwanda cha kuchakata ngozi ili kuongeza thamani ya bidhaa hiyo na pato la taifa.

Rai hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha, wakati alipofanya ziara katika machinjio hayo mwishoni mwa wiki kwa lengo la kuona shughuli zinazofanywa.

“Serikali hii tupo tayari kuwasaidia kuanzisha kiwanda hicho kwa kuongea na mifuko ya hifadhi ya jamii ili wawekeze kwani eneo kubwa lipo na halitumiki," alisema.

Aliutaka uongozi wa machinjio hayo pia kungalia jinsi ya kuchakata mifupa pamoja na damu ya mifugo kwa ajili ya kuzalisha vyakula vya kuku badala ya kuvitupa vitu hivyo.

Pia aliutaka uongozi huo kuangalia namna ya kuongeza thamani ya nyama inayochinjwa katika machinjio hayo kwa ajili ya kuvutia soko la walaji.

Alisema Tanzania ni nchi ya pili katika bara la Afrika kwa wingi wa mifugo, lakini haina viwanda vya kuchakata ngozi na kwamba ngozi inayotumika katika gereza la Karanga mkoani Kilimanjaro inatoka nchini Kenya.

Alisema mifugo mingi ya Tanzania inauzwa nchini Kenya na kuongeza halmashauri za nchi hiyo kipato, huku halmashauri za Tanzania haswa katika ukanda wa Kaskazini zikikosa mapato.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa machinjio hayo, Joseph Singuya, alisema yana uwezo wa kuchinja ng’ombe kati ya 400 mpaka 500 kwa siku.

Habari Kubwa