Madereva Bajaj walia na ada, faini

29May 2019
Na Mwandishi Wetu
MOSHI
Nipashe
Madereva Bajaj walia na ada, faini

BAADHI ya madereva pikipiki zenye magurudumu matatu (Bajaj) katika Manispaa ya Moshi, wameulalamikia uongozi wa manispaa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kwa kushindwa kusimamia maegesho ya pamoja na uwekwaji wa namba, hivyo kusababisha ugumu kufanya biashara hiyo.

bajaji.

Mmoja wa madereva hao, Frank Simon, alisema mbali na manispaa kushindwa kutoa utaratibu wa maegesho, pia kumekuwapo na chama ambacho hakitambuliki kisheria kinachowalazimisha wamiliki na madereva kujiunga kwa kiingilio cha Sh. 12,000, huku Sumatra wakitaka 10,000/-

Alisema mbali na kuwataka wa walipe Sh. 22,000 kwa mamlaka hizo mbili, pia wamekuwa wakipewa risiti za mkono hali inayoashiria ni ukiukwaji wa ulipwaji wa mapato.

"Sisi ni watafutaji wadogo wa pesa halali, lakini tunanyanyaswa na serikali kupitia viongozi wa Manispaa na Sumatra kwani hawatoi elimu sahihi ya nani anasimamia nini. Hali hii inasababisha mkoanganyiko mkubwa una upigwaji wa fini za mara kwa mara kwa kutumia chama hicho kisichotambulika na viongozi wake hatujawachakua sisi.

Zaidi kabisa wanatoa risiti za mkono hali ambayo inaashiria kuna hujuma zinatendeka," alisema.

Naye Amos Lukas alisema: “Mbali na Sh. 12,000 ya kujiunga na kikundi ambacho hatukitambui pia tunalazimika kulipa Sh. 10,000 kwa ajili ya kuchorewa namba inayotoka Sumatra kinyumbe cha taratibu na sheria za nchi."

Mmoja wa abiria wanaotumia usafiri wa Bajaj, Ismail Kondo, alikiriki kunyanyaswa kwa baadhi ya madereva hao na kuiomba serikali kuhakikisha wanalifanyia kazi kwa uwazi na ukweli ikiwa ni pamoja na kuchukuwa hatua stahiki kwa watendaji wote wanokiuka matumizi ya mashine za kielektroniki ( EFD).

Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa wa Kilimanjaro, Jones Makwale, alikanusha madai hayo kwa kusema ulipwaji wa pesa za Sumatra unatumika kwa njia zilizoainishwa kisheria na risiti za kielektroniki zinatolewa.

Habari Kubwa