Madini Nickel kuichangia Ngara bil. 151/-

23Jun 2022
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Madini Nickel kuichangia Ngara bil. 151/-

BUNGE limeelezwa uchimbaji wa madini ya Nickel utachangia ushuru wa huduma kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara mkoani Kagera takribani Sh. bilioni 151 kwa kipindi cha uhai wa mgodi.

Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ngara (CCM), Ndaisaba Ruhoro.

Mbunge huyo alisema, mpango wa serikali kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Ngara wananufaika na uchimbaji wa madini ya Nickel unaotarajia kuanza eneo la Kabanga.

Akijibu, Dk. Kiruswa alisema uchimbaji wa madini ya Nickel katika eneo la Kabanga unafanywa na Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited iliyopewa leseni Oktoba 25, 2021.

“Mradi huo unatarajia kuchangia ushuru wa huduma kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, kiasi cha Dola za Marekani milioni 65, sawa na takribani Sh. bilioni 151 kwa kipindi cha uhai wa mgodi,” alisema.

Alisema mradi huo unatarajia kutoa ajira za moja kwa moja 978.

“Hadi kufikia Aprili, 2022 mradi ulikuwa umetumia jumla ya Dola za Marekani milioni 1.5 katika ununuzi wa bidhaa na huduma ndani ya nchi. Kati ya hizo, Dola za Marekani 125,673 zilitumika kufanya ununuzi katika Wilaya ya Ngara,” alisema.

Alitoa rai kwa wananchi wa Wilaya ya Ngara na taifa kwa ujumla kuchangamkia fursa zilizoko katika mradi huo.
“Kupitia Sheria ya Wajibu wa Makampuni kwa Jamii (CSR), mradi huo ulichangia takribani Sh. milioni 39 kwa mwaka 2021 na unatarajia kuchangia Sh. milioni 207.8,” alisema.

Katika swali la nyongeza, mbunge huyo alihoji kama Wizara ya Madini ina tafiti zilizofanywa na wakoloni za madini ili kuwekwa wazi kwa Watanzania wawekeze.

Dk. Kiruswa alijibu kuwa Wajerumani walipofanya utafiti wa madini nchini waliacha takwimu za kutosha na zipo kwenye wizara hiyo.

Alitoa rai kwa Watanzania wenye nia ya kuwekeza kwenye madini taarifa zipo za tangu mwaka 1925 wazifuatilie ili kuwaongoza kwenye uchimbaji wa madini husika kwenye maeneo yaliyofanyiwa utafiti.