Madiwani waukataa mradi duni wa maji

27Jan 2019
Jumbe Ismaily
IKUNGI
Nipashe Jumapili
Madiwani waukataa mradi duni wa maji

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida limeikataa taarifa ya ukarabati na upanuzi wa mradi wa maji Iyumbu, uliogharimu jumla ya Shilingi milioni 71.6.

MRADI WA MAJI IKUNGI

Taarifa iliyotolewa kwenye mkutano huo ilisema wameigomea kwa  kuwa haina ukweli kutokana na mradi huo kuwa na upungufu ambao unahitaji kukamilishwa.

 

Aidha, kufuatia upungufu huo, baraza hilo limemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Justice Kijazi, kutomlipa mkandarasi wa mradi huo malipo ya mwisho ya fedha zilizobakia hadi hapo atakapokamilisha kazi na kurekebisha upungufu uliogundulika.

 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga, alitoa maagizo  hayo kwenye mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa kujadili bajeti ya mwaka wa fedha wa 2019/2020.

 

 Mwanga ambaye pia ni diwani wa kata ya Irisya, alikiri kwamba kuna baadhi ya kazi hazijafanywa na mkandarasi huyo.

 

Kwa mujibu wa Mwanga katika kikao cha kamati ya kudumu walikubaliana kwamba iwapo mkandarasi wa mradi huo hajakabidhi kazi asilipwe  fedha kwanza mpaka atakapokamilisha mradi.

 

 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya hiyo,Justice Kijazi licha ya kukiri kuwepo kwa hoja hiyo katika taarifa za mkaguzi , aliahidi kuchukua hatua zaidi.

 

Halima Athumani diwani wa viti maalumu alisisitiza kwamba katika ziara yake aliyotembelea Iyumbu alishuhudia kutofanyika kwa ukarabati uliotakiwa zaidi ya kupakwa rangi huku kukiwa na manyigu yametanda kwenye mashine za maji.

 

“Katika ukarabati na upanuzi wa mradi wa maji Iyumbu, ambao umetumia milioni 71.6 awali ulikuwa umetengewa Shilingi milioni 79.6, leo  unadaiwa umekamilika lakini katika taarifa ya kamati ya jumuiya ya watumia maji inaelezwa kuwa  mashine haijakarabatiwa na hakuna matengenezo yeyote ya pampu na injini ya dizeli yaliyofanyika ”alisisitiza diwani huyo wa viti maalumu.

Diwani wa kata ya Iyumbu, Peter Kuligwa alionyesha kusikitishwa na utaratibu unaotumiwa na wataalamu wa kupeleka miradi kwenye kata huku ushiriki wa madiwani ukiwa ni wa asilimia ndogo na kwamba mara nyingi hawaelimishwi  shughuli za kitaalamu zitakazofanyika.

 

 

Habari Kubwa