Maduka 28 ya pembejeo yaanzishwa Nyanda za Juu

13Oct 2021
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Maduka 28 ya pembejeo yaanzishwa Nyanda za Juu

MADUKA 28 ya pembejeo za kilimo yameanzishwa mikoa ya Nyanda ya Nyanda za Juu Kusini lengo likiwa kuwasaidia wakulima kupata mbegu na mbolea bora kwa wakati.

Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Ekari Moja Tanzania, Dorcas Tinga, alisema hayo wakati wa uzinduzi wa maduka 12 kati ya 28 ambayo yamezinduliwa mkoani hapa.

Alifafanua kuwa maduka 16 yalifunguliwa mkoani Njombe, tisa na matatu Songwe, yote yanakidhi vigezo vya utoaji huduma bora za pembejeo za kilimo.

“Katika kuhakikisha Kampuni yetu inamjali mkulima tulianzisha programu ya kuwakopesha wakulima pembejeo za kilimo pamoja na mafunzo ili wazalishe kwa tija na kwamba hadi sasa wakulima 60,000 wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wamenufaika,” alisema Tinga.

Miongoni mwa wakulima wanaonufaika na kampuni hiyo, Teresia Mponzi kutoka Imezu, alisema elimu ya kilimo bora imekuwa msaada kwao kwa sababu wanalima kwa tija na kujiongezea kipato.

Aliiomba Kampuni ya Ekari Moja kuendelea kutoa mikopo yenye riba nafuu na elimu ili wakulima wanufaike na kujikwamua kiuchumi.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Rashid Chuachua, alisema serikali imetoa maelekezo kwa halmashauri zote kwa ajili ya kuimarisha sekta ya kilimo na kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga Sh. bilioni 187 kuimarisha kilimo nchini.

Aliipongeza Kampuni ya Ekari Moja kuwekeza katika utafiti na teknolojia ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wakulima kwa kuanza na vijiji vitatu vyenye wakulima 433 mwaka 2016.

Alisema hadi sasa jumla ya wakulima 6,957 wa vijiji 37 kwenye msimu wa kilimo 2021/2022 wamenufaika na wanaendelea kupata tija na manufaa kutoka kampuni hiyo.

Habari Kubwa