Maduka yafungwa kisa bei vifaa vya kujikinga corona

25Mar 2020
Godfrey Mushi
Hai
Nipashe
Maduka yafungwa kisa bei vifaa vya kujikinga corona

MADUKA makubwa matatu yanayouza vifaa muhimu vya kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu, yamefungwa wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, baada ya kubainika kuuza barakoa na vitakasa mikono kwa bei kubwa.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya, alithibitisha jana kuwa serikali kuchukua hatua hiyo ili kunusuru wanyonge dhidi ya unyonyaji kupitia bei ya vifaa hivyo.

“Tumeshayafunga maduka matatu katikati ya mji na hivi sasa bei ya kawaida imerejea katika maduka yote yenye 'masks' (barakoa) na 'hand sanitizers' (vitakasa mikono) katika wilaya yetu.

"Bado tunatafakari tutayafungua lini maduka hayo, lakini tunatafakari wamekosa utu kiasi gani kwa kufanya biashara ya ulanguzi wakati watu wako kwenye tahadhari," alisema.

Wiki iliyopita, Ole Sabaya aliamuru kukamatwa kwa wafanyabiashara watakaobainika kupandisha bei ya vifaa hivyo na kutaka maofisa biashara kufanya uchunguzi wa kimyakimya na watakapobaini, wachukue hatua ya kuyafunga maduka yote ambayo yatabainika kupandisha bei ya barakoa na vitakasa mikono.

Pia, aliagiza kufanyika kwa ukaguzi wa dharura kila siku katika maduka yanayouza vifaa vya kujikinga na maambukizo ya homa hiyo inayosababishwa na virusi vya corona.

Bei ya kawaida ya vitakasa mikono katika Wilaya ya Hai kwa sasa ni Sh. 2,500 na maski inauzwa kwa Sh. 2,000.

Kabla ya serikali kutangaza adhabu ya kuyafunga maduka yatakayobainika kupandisha bei, vitakasa mikono vilipaa sokoni kutoka bei ya Sh. 2,500 na kuuzwa kati ya Sh. 10,000 hadi 15,000 kwa pea moja.

Pia, majitiba yalikuwa yakiuzwa kwa Sh. 10,000, lakini bei yake ilipanda na kuuzwa kati ya Sh. 20,000 na Sh. 25,000.

Ugonjwa huo huambukizwa kwa njia ya hewa kwa kuingiwa na majimaji yenye virusi kutoka kwa mtu mmoja kwa njia ya kukohoa au kupiga chafya au kwa kugusa majimaji au kamasi kutoka kwa mtu mwenye virusi hivyo.

Dalili za ugonjwa huo, huanza kuonekana kati ya siku moja hadi 14 tangu kupata maambukizo.

Habari Kubwa