Maelfu wanufaishwa mafunzo stadi za kilimo

28Jul 2021
Elizaberth Zaya
Morogoro
Nipashe
Maelfu wanufaishwa mafunzo stadi za kilimo

WAKULIMA 2,176 wakiwamo wanawake 1,294 na wanaume 882 wa mikoa ya Morogoro, Iringa na Njombe wamenufaika na mafunzo ya stadi katika kilimo na ufugaji yaliyotolewa kupitia mradi wa Tajirika na Kilimo unaotekelezwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Shirika la Kimataifa la ....

CARE na Taasisi ya Ukuzaji Kilimo Uwanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).

Akizungumza wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo, Mratibu wa mradi huo kutoka VETA, Perecy Ugula, alisema wakulima hao walipatiwa mafunzo ya ufugaji bora wa mifugo hususani ng’ombe wa maziwa na kuku, kilimo cha mazao mchanganyiko, na cha mboga na matunda.

Ofisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Shirika la Kimataifa la CARE, Edwin Sallu, alisema kupitia utekelezaji wa mradi huo, wamegundua uwapo wa uhitaji mkubwa wa mafunzo stadi za kuboresha shughuli za kilimo kwa wakulima wadogo vijijini.

Sallu alisema mafunzo hayo yamesaidia kuunda vikundi 141 vya uzalishaji katika sekta ya kilimo cha mazao mchanganyiko, mboga na matunda na ufugaji wa kibiashara na kwamba kwa sasa wanafanya shughuli zao za kilimo kwa umoja, hali inayowezesha uzalishaji mazao kwa wingi, ubora na uhakika wa kufikia masoko ya bidhaa zao pamoja na kukopesheka kwa urahisi na kupata faida.

“Kwa kweli tumeshuhudia manufaa makubwa ya mafunzo yaliyotolewa kupitia mradi huu kwa wakulima vijijini, hasa ukizingatia kuwa asilimia 67 ya wanufaika ni wanawake na watoto wa kike ambao tunaamini wataleta mabadiliko chanya kwenye jamii zao,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Kejeri Gillah, alishauri kuweka mkakati wa uendelezaji wa shughuli zilizofanywa kwenye mradi huo ili wakulima wengi zaidi wanufaike na mafunzo hayo.

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Nyanda za Juu, Susan Magani, alisema mamlaka hiyo inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi yanawafikia wananchi wengi zaidi hasa maeneo ya vijijini na kwamba anaamini kuwa wakulima wengi zaidi nchini watanufaika na mafunzo hayo ili kuboresha shughuli zao.

Mradi wa Tajirika na Kilimo ulianza kutekelezwa mwaka 2018 kwa lengo la kujenga na kuimarisha ujuzi katika sekta ya kilimo kwa wakulima 2,200 na unatarajiwa kumalizika Desemba mwaka huu.

Habari Kubwa