Maelfu ya ng’ombe waogeshwa kijijini

16Jan 2019
George Tarimo
Mufindi
Nipashe
Maelfu ya ng’ombe waogeshwa kijijini

BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Gamaa wilayani Mufindi mkoani Iringa, wamesema wanapoteza mifugo mingi kutokana na kushambuliwa na baadhi ya magonjwa ikiwamo ndiganakali na kupe.

Mkuu wa wilaya ya Mufindi, Jamhuri William, PICHA MTANDAO

Wakizungumza baada ya kumalizika zoezi la kuogesha zaidi ya ng’ombe 2,000 katika kijiji hicho, walisema wameamua kuogesha mifugo yao kwa lengo la kumaliza magonjwa yanayowasumbua kwa muda mrefu.

Walisema magonjwa hayo yanachangia mifugo kufa. Kijiji cha Gamaa kina zaidi ya mifugo 10,000, huku idadi kubwa ya wakazi wa eneo hilo wanategemea shuguli za kilimo na ufugaji.

Walisema baada ya kuogesha mifugo yao, huenda ikawa salama kutokana na kupata tiba.

Husen Kadege, Gospal Mboniko na Festo Mutweve, walisema awali mfugaji mmoja alikuwa na mifugo mingi, lakini kila siku ng’ombe wanne au watatu walikuwa wanakufa na baada ya serikali kuona tatizo hilo wamewapatia tiba ili kunusuru vifo vya mifugo yao na sasa vifo vimepungua.

Mboniko alisema walikuwa wakiogesha kienyeji, lakini baadaye walipata elimu, hivyo sasa wanaogesha kisasa jambo ambalo limesaidia kupunguza vifo vya mifugo.

Mutweve alisema athari zilikuwa kubwa kwa sababu huduma za matibabu zilikuwa changamoto kwa wafugaji kwa maana mifugo mingi ilikuwa ikipoteza uhai kutokana na kutokuwapo tiba.

Ofisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Robart Simaganga, alisema katika halmashauri hiyo wanakabiliwa na magonjwa manne sugu ambayo ni ndiganakali, ndigana baridi, maji ya mori ambayo yana dalili ya mifugo kukojoa damu pamoja na homa za kupe.

“Kwa jitihada hizi za uzinduzi wa uogeshaji, tunaamini huu ni mwanzo wa wafugaji kuogesha mara kwa mara na nawataka wafugaji kutunza josho hili,” alisema na kuongeza:

“Huu msingi waliopewa na serikali ni wa kuuendeleza, lakini pia takribani ng’ombe 2,172 wameogeshwa bure katika josho hili.”

Mkuu wa wilaya ya Mufindi, Jamhuri William, aliwataka viongozi wa vijiji kutunza mazingira na kutokaribisha wafugaji ilhali maeneo ya ufugaji ni madogo.

Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ina jumla ya majosho 41 yanayofanya kazi na kati ya hayo majosho 36 yanaendeshwa na vikundi vya wafugaji chini ya umiliki wa serikali na majosho matano yanamilikiwa na taasisi za watu binafsi.

Habari Kubwa