Maendeleo kufika  haraka zaidi

16Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Maendeleo kufika  haraka zaidi

KUTOKANA na ruzuku ndogo kutoka Serikalini, Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga imeamua kutoa fedha zake za ndani kusaidia katika miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shegela.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mussa Semdoe aliyasema hayo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shegela alipotembelea wilayani humo kukagua miradi ya maendeleo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Semdoe alibainisha kwamba Halmashauri hiyo inajikita katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ili fedha hizo zisaidie kutatua baadhi ya changamoto katika maendeleo ya jamii ambapo tayari wamekwisha toa kiasi cha fedha kusaidia katika sekta ya elimu.

“Tumeshaanza kutoa takribani Sh. milioni 200 katika kusaidia shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa," alisema Semdoe kwa sababu "ruzuku inayokuja kutoka Serikalini ni ndogo".

"Hivyo tumeamua kutoa fedha zetu za ndani ili kusaidia nguvu za wananchi.”

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sauda Mtondoo aliwataka wazazi na walimu kuhakikisha wanawapatia elimu inayostahili wanafunzi wilayani humo ili kuongeza kiwango cha ufaulu na pia kuwapatia watoto hao haki zao za msingi kielimu.

Aidha, Mtondoo aliwataka viongozi wa vijiji na watendaji wa kata kusimamia na kufuatilia suala zima la elimu kwenye kata zao na kila baada ya wiki moja wapeleke ripoti katika ofisi yake ili kuhakikisha wanasaidia kuongezeka kwa ufaulu ndani ya wilaya hiyo.

“Katika wilaya yetu ufaulu unaongezeka mwaka hadi mwaka, lakini wito wangu kwa walimu waongeze bidii na weledi kuhakikisha wanatoa elimu bora na kuwasaidia watoto ili waendelee kufanya vizuri, na hii kwa walimu wote wa msingi na sekondari” alisisitiza Mtondoo.

Habari Kubwa