Mafunzo TBS yadhihirisha mkakati kufukia lengo la Tanzania ya viwanda

26Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Tanga
Nipashe
Mafunzo TBS yadhihirisha mkakati kufukia lengo la Tanzania ya viwanda

SERIKALI mkoani Tanga imesema mafunzo yanayotolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa wafanyabiashara kuhusu usajili wa majengo na bidhaa za chakula na vipodozi ni uthibitisho wa azma ya serikali kufanikisha malengo ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Judica Omary, alisema hayo jana wakati akifungua mafunzo yanayoendeshwa na shirika hilo kwa wajasiriamali kuhusiana na usajili wa majengo na bidhaa za chakula na vipodozi.

Alisema uongozi wa mkoa unaamini kuwa mafunzo hayo ni njia mwafaka ya kuleta tija zaidi katika juhudi za kuliletea taifa maendeleo ya haraka kulingana na fursa zilizopo hasa kwenye sekta za viwanda, kilimo, biashara, uvuvi na maeneo mengine mengi.

"Mafunzo haya yamekuja kwa wakati mwafaka ambapo serikali imeazimia kwa dhati kabisa kuendeleza viwanda ili kutoa ajira katika kada mbalimbali pamoja na kuziwezesha bidhaa zetu kushindana katika masoko ya ndani, kikanda na nje ya Tanzania," alisema Omary.

Alisisitiza kwamba wanaona mwelekeo mzuri chini ya usimamizi wa Rais John Magufuli ambao umewezesha nchi kutoka katika uchumi wa chini na sasa imeingia uchumi wa kati.

"Nchi yetu kuwa na uchumi wa kati imekuwa chachu ya kutufanya tuendelee kufanya kazi kwa bidii na maarifa kwa hiyo tusibweteke. Ni muhimu washiriki wa mafunzo haya msikilize kwa makini na kuchangia mada hizi kwa uwazi ili kupata utaalamu mtakaoutumia kwenye shughuli zenu," alisema.

Alifafanua kwamba ni imani yake kuwa baada ya mafunzo hayo watakuwa wamepata elimu, itakayowawezesha kusajili maeneo ya shughuli zao za biashara.

Aliwataka washiriki kutumia fursa hiyo kujadili kwa pamoja na wataalamu changamoto mbalimbali zinazohusiana na huduma zinazotolewa na TBS zikiwemo taasisi zingine zikiwamo Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Ofisi ya Ofisa Biashara, Afya na Maendeleo ya Jamii.

Kwa upande wa Tanga, Omary alisema TBS inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na watendaji walioko katika kalmashauri ili kurahisisha kufikisha huduma kwa wananchi.

"Kwa hiyo nazielekeza halmashauri zote za mkoa wa Tanga kuendelea kutoa ushirikiano kwa TBS iii kuwahudumia wananchi wetu kwa ufanisi na kwa haraka," aliagiza.

Alitoa mwito kwa shirika hilo kuendelea kuongeza nguvu katika kuboresha uhusiano huu na halmashauri za mkoa huo hasa kwa kushirikiana kwa karibu na Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri.

Mafunzo hayo yanalenga kutoa uelewa kuhusu taratibu za usajili wa majengo na bidhaa za chakula na vipodozi, madhara ya vipodozi vyenye viambata sumu pamoja na kufanya usajili wa majengo yanayohusiana na shughuli za uzalishaji, utunzaji na uuzaji wa bidhaa za chakula na vipodozi hususan kwa yale ambayo hayajafanyiwa usajili au muda wa usajili uliofanywa awali ulifikia ukomo.

Kundi lililolengwa kwa ajili ya mafunzo hayo ni wajasiriamali ambao ni sehemu muhimu katika sekta binafsi inayochangia pato la taifa, kuongeza ajira na kuondoa umasikini nchini.

Habari Kubwa