Mafuta ya magendo ya mil. 70/- yalivyonaswa

06Apr 2017
Said Hamdani
KILWA MASOKO
Nipashe
Mafuta ya magendo ya mil. 70/- yalivyonaswa

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, imekamata madumu 1,327 ya mafuta ya kula yenye thamani ya Sh. 70,331,000 yakiingizwa kinyemela na wafanyabiashara ambao hawajafahamika, kwa lengo la kukwepa ushuru.

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Lindi, Masawa Masatu, alieleza jinsi mafuta hayo yalivyokamatwa alipokuwa akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, alipotembelea ofisi ya mamlaka hiyo.

Kwa mujibu wa Masatu, mafuta hayo yalikamatwa usiku wa Aprili mosi, 2001, yakiwa yametelekezwa vichakani katika bandari bubu inayofahamika kwa jina la Gombawana katika Kijiji cha Mnago, Kata ya Kivinje-Singino.

Masatu alisema kukamatwa kwa mafuta hayo kumetokana na TRA kupewa taarifa kutoka kwa raia wema, na walipofuatilia kuliyakuta madumu hayo huku wahusika wakitoroka.

“Baada ya kupewa taarifa, tuliongozwa na askari polisi usiku huo kuelekea eneo hilo na kufanikiwa kuyakuta yakiwa yametelekezwa vichakani,” alisema na kuongeza kuwa mafuta hayo aina ya Mico Gold na Viking, yametengenezwa Malaysia na Indonesia.

Alieleza kuwa kama mafuta hayo yangeingia sokoni na kuuzwa, Serikali ilikuwa imepoteza ushuru wa Sh. 16,900,000.

Kwa upande wake DC Ngubiagai aliwataka wafanyabiashara kuwa wazalendo ikiwa ni pamoja na kuacha tabia ya kutumia bandari bubu kupitishia bidhaa wanazoziagiza, kwa lengo la kukwepa ushuru wa serikali.

Ngubiagai amesema kulipa kodi na ushuru kunaiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake ya maendeleo, ikiwamo utengenezaji wa miundombinu ya barabara, upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa matumizi ya binadamu na upatikanaji wa dawa hospitalini.

Aidha, alisema vitendo vya baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi na ushuru, vinawakatisha tamaa wenzao wanaofuata sheria na taratibu, ikiwamo kulipa ushuru, kodi na kukata leseni.

Habari Kubwa