Magari ya umeme yaanza kutumika hifadhini

10Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
ARUSHA
Nipashe
Magari ya umeme yaanza kutumika hifadhini

MAGARI yanayotumia nguvu ya umeme yameanza kutumika kwa ajili ya kusafirishia watalii katika hifadhi za taifa zilizoko katika ukanda wa kaskazini baada ya kubadilishwa kutoka katika mfumo wa kutumia mafuta ya dizeli na petroli.

Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA Jenerali Mstaafu George Waitara ( kulia) akimkabidhi Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla Tuzo iliyopewa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kuwa hifadhi Bora katika Bara la Afrika kwa mwaka 2019.

Hayo yamebainika katika maonyesho makubwa ya utalii katika eneo la Afrika ya Mashariki yanayofahamika kama Karibu-Kili Far yaliyomalizika jana mjini hapa.

Ukanda wa utalii wa kaskazini unaundwa na hifadhi ya taifa ya Arusha, Kilimanjaro, Ziwa Manyara, Serengeti, Tarangire na Mkomazi pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA).

Akikagua mabanda mbalimbali ya utalii, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, alielezwa na Mwenyekiti wa mradi unaobadilisha mfumo wa magari na kuweka wa umeme wa E-Mission Afrika, Satbir Hanspaul, kwamba magari hayo ni rafiki kwa mazingira ya mbuga za wanyamapori.

“Lazima tuungane na serikali pamoja na wadau wengine katika kuhakikisha tunalinda na kutunza mazingira huko porini katika hifadhi zetu za taifa,” alisema.

Hanspaul alisema matumizi ya mfumo wa umeme unayafanya magari yasitoe moshi au gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani ikiwamo hewa ya ukaa na ambazo ni hatari kwa mazingira.

Aidha, alisema kuwa faida nyingine ya magari hayo ni kutokuwa na kelele na hivyo kuleta utulivu na ustawi mkubwa wa wanyamapori katika hifadhi za taifa.

Alisema baada ya kuchaji vizuri, gari inauwezo wa kwenda kilometa 180 kwa mwendokasi wa zaidi ya kilometa 100 kwa saa moja.

“Hii ni teknolojia mpya ambayo ni nafuu kuliko ya kutumia diseli au petroli kwa kuwa baada ya kuibadilisha gari hakuna gharama kubwa na hata kulifanyia gari matengenezo baada ya kwenda umbali fulani, haitahitaji mambo mengi na utaweza kudumu nayo kwa miaka zaidi ya 20,” alisema.

Hanspaul alisema wanaangalia uwezekano wa kuwa na vituo vya kuchajia umeme hasa kwenye vituo mbalimbali vya kujaza mafuta ya magari hasa kwa kuanzia katika maeneo ya hifadhi za taifa za ukanda wa kaskazini.

Alisema kwa upande wa msaada ya kiufundi, tayari wameweka vituo vya uhakika katika maeneo mbalimbali aliyoyataja kuwa ni Hifadhi ya taifa ya Ziwa Manyara na Hifadhi ya Serengeti katika eneo la Seronera lilipo kaskazini mwa  hifadhi hiyo, katika eneo la Kogatende na kusini katika eneo la Ndutu.

Hanspaul alisema  mfumo huo umekuwa na mafanikio makubwa kwa injini ya gari aina ya Landcruiser, huku akifafanua  wapo katika hatua ya mwisho kwa injini ya magari aina ya Landrover.

Hata hivyo Hanspaul alieleza hivi sasa wanayafanyia kazi magari yote ambayo yana injini inayozungusha magurudumu yote ambayo ndiyo kwa kawaida usafirisha watalii kwenda mbugani.

Alisema kuwa baada ya kukamilisha kubadilisha injini ya magari makubwa ya utalii wataingia katika magari ya kawaida yanayotumiwa mijini kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Watumiaji wa awali wa magari hayo wanaeleza yana mfumo wa kuhifadhi nguvu ya umeme wa aina tatu, ambapo wa kwanza una uwezo wa umeme  kwa saa nane, wa pili saa nne na wa tatu ukiwa na uwezo wa kuhifadhi umeme kwa saa mbili na robo.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Equtorial, Roman Chuwa, alisema matumizi ya mfumo wa umeme unaweza kuwa nafuu zaidi endapo baadhi ya maeneo yataweza kuwa na mfumo wa kuyajaza umeme magari hayo unaotumia nishati ya jua.

Naye Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), William Mwakilema, alisema  kuingia kwa teknolojia ya magari ya aina hiyo ni mapinduzi makubwa ya uhifadhi kwa kupunguza hewa ya ukaa inayotokana na moshi wa magari.

 Mradi wa E-Mission Afrika unatekelezwa na kampuni ya maarufu nchini kwa kurefusha bodi ya magari ya utalii ya Hanspaul Automechs Limited kwa kushirikiana na Gadgetronix Limited yote ya jijini Arusha.

Habari Kubwa