Magazeti yote IPP yapata leseni mpya

14Sep 2017
Halima Kambi
Nipashe
Magazeti yote IPP yapata leseni mpya

KAMPUNI ya The Guardian Limited (TGL), ambayo ni moja ya kampuni zilizo chini ya IPP Limited, imepata leseni ya magazeti yake 10, baada ya kukamilisha taratibu za usajili upya wa machapisho hayo.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, akimkabidhi leseni ya usajili wa Gazeti la Nipashe, Meneja Sheria na Mahusiano wa kampuni ya The Guardian Ltd, Emmanuel Matondo (kulia), jijini Dar es Salaam jana. PICHA: HALIMA KAMBI

Usajili huo mpya wa magazeti unatokana na kuanzishwa kwa Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 (Media Service Act 2016), kama ilivyotangazwa na serikali hivi karibuni.

Magazeti ya TGL ambayo yalipata usajili jana ni The Guardian, The Guardian On Sunday, Nipashe, Nipashe Jumapili, ThisDay, Kulikoni, Alasiri, Taifa Letu, Lete Raha na Sema Usikike.
 
Akikabidhi leseni hizo kwa Mhariri Mkuu wa TGL, Jesse Kwayu, aliyefuatana na Mwanasheria wa Kampuni hiyo, Emmanuel Matondo, jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo, Dk. Hassan Abbas, alisisitiza jana kuwa muda wa mwisho uliowekwa na serikali kwa kila mmiliki wa gazeti kusajili upya ukifika, hautaongezwa.

“Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari watumie muda huu uliowekwa wa kusajili upya magazeti. Muda huu ukimalizika,” alisema.

Muda wa mwisho wa kufanya usajili ni Oktoba 15, mwaka huu huku Dk. Abbas akiipongeza TGL kwa kufanikisha usajili wa magazeti yake kwa wakati.

Aliwataka wamiliki wengine kutumia muda uliopo kukamilisha kazi hiyo kwa kuwa sheria haitaruhusu chapisho lolote ambalo halijasajiliwa upya baada ya kumalizika kwa muda uliowekwa.

“Leo nimefurahi sana natoa cheti cha usajili kwa gazeti ambalo niliwahi kuwa mhariri wake ambalo ni Kulikoni,” alisema Dk. Abbas.
 
Naye Kwayu aliishukuru Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ushirikiano walioutoa kwa TGL kwa kufanikisha kuwapatia usajili kwa wakati.

Aliomba ushirikiano huo uendelezwe kwa wamiliki wengine, ili kusaidia ustawi wa magazeti na uhuru wa habari nchini kwa ujumla.

Habari Kubwa