Magendo mifugo yainyima serikali mapato

27Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Longido
Nipashe Jumapili
Magendo mifugo yainyima serikali mapatoSERIKALI imekuwa ikipoteza mapato ya kati ya Sh. bilioni nne hadi tano
kwa mwaka, kufuatia uuzwaji wa mbuzi kwa magendo kupelekwa 
Kenya.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe. 
Alisema serikali imekuwa ikikosa mapato ya Sh. bilioni nne hadi tano kwa kipindi cha miaka mingi kutokana na mifugo hiyo kwenda kuuzwa Kenya, kupitia mpaka wa Namanga.


Hata hivyo, alisema serikali hadi kufikia mwaka jana wamefanikiwa kudhibiti uuzwaji wa mifugo nje ya nchi ili kuokoa fedha zilizokuwa zinapotea.

“Mbuzi walikuwa wakiuzwa kwa njia za magendo na njia halali, lakini
njia ya magendo ilikuwa ikiuza mbuzi wengi zaidi, tumechukua hatua kama
serikali ya kudhibiti na tumekuwa wakali sana na tumeshaeleweka sasa
mambo yanakwenda vizuri,” alisema Mwaisumbe.Alisema ilibidi serikali kuwa wakali ili kurudisha hali ya
uhalali wa biashara ya mbuzi na wakati mwingine walikuwa wakitaifisha
mifugo iliyokamatwa kutoka kwa wafanyabiashara waliokuwa wakiuza kwa njia za magendo.“Tukikamata mbuzi na kugundua wanauzwa kwa magendo tunawataifisha maana siwezi kuona serikali inakosa mapato kutokana na tamaa za watu
wachache, suala hili niko makini naomba wafanyabiashara wanielewe,
mapato ndio yanamsaidia Rais John Magufuli katika juhudi zake za
kuelekeza Watanzania kwenye uchumi wa kati na kupunguza
umaskini,” alisema Mwaisumbe.Hata hivyo, Mwaisumbe alisema ameshawezesha wafanyabiashara hao,
kuunda vikundi vya watu kati ya 30 hadi 45 na kuvirasimisha ili kukaa
kwa kuangalia mianya ya upotevu wa mapato ya serikali, sambamba na kufanya tathmini ya mafanikio ya wafanyabiashara.


Alisema vikundi hivyo vitawasaidia kuwa na umoja ambao utaunganisha nguvu za pamoja na hata kusafirisha kwa pamoja mbuzi hao, kwa njia halali ili
nchi ipate kodi kwa ajili ya maendeleo ya watu wake wakiwamo wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo.


“Tumedhibiti kwa asilimia 90 uuzwaji holela wa mbuzi wa magendo, lakini kwa ushirikiano wa pamoja, wafanyabiashara matarajio yetu ni kufikia
asilimia 100,” aliongeza Mwaisumbe.

Habari Kubwa