Magereza zalisheni viatu, bidhaa bora

13Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Moshi
Nipashe Jumapili
Magereza zalisheni viatu, bidhaa bora

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Jenista Mhagama, amewataka watendaji wa kiwanda cha viatu na bidhaa za ngozi kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kuvutia wateja wa nje na ndani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Jenista Mhagama (katikati), akipata maelekezo viatu vinavyotengenezwa kwa ngozi kutoka kwa Afisa Masoko wa kiwanda cha Viatu cha Gereza la Karanga, Fredrick Njoka (kushoto), wakati wa ziara yake kiwandani hapo, mjini Moshi mkoani Kilimanjaro jana. PICHA: OWM

Alitoa maagizo hayo alipotembelea kiwanda cha Karanga kinachomilikiwa na gereza la Lukaranga kilichopo wilaya ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro, kukagua shughuli za uendeshaji na uzalishaji.

“Niwatake watendaji kuweka mikakati madhubuti ya kuendelea kutengeneza bidhaa zenye ubora kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa”, alisema Mhagama

Aidha Waziri aliwaasa watendaji wa kiwanda hicho kuendelea kutatua changamoto zinazowazunguka za kimfumo kwa kuzingatia sheria na taratibu za uendeshaji wa kiwanda hicho ili kuendana na ukuaji wa teknolojia na ushindani ulipo.

“Nisingependa kuona kiwanda kinakwama kuzalisha bidhaa zenye ubora, hivyo ni vyema kuzingatia sheria na kanuni za uendeshaji wa kiwanda katika ufanisi wa hali ya juu”,alisisitiza Mhagama.

Waziri alieleza kuwa, ili kuwa na wateja wa uhakika ni vyema kutumia mbinu za kujitangaza juu ya shughuli na bidhaa zinazozalishwa kwa kutumia vyombo vya habari ili kuendana na soko lililopo nchini.

Aidha, Waziri alieleza mpango mkakati wa ujenzi wa kiwanda kikubwa eneo hilo la gereza la Karanga na tayari eneo limetengwa kwa ajili ya ujenzi na kuboresha kiwanda kilichopo ili kuongeza uzalishaji kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

“Uwekezaji unalenga kuboresha kiwanda cha zamani kutoka kuzalisha jozi 150 kwa siku hadi 400 ingawa mpango mkakati uliopo ni kuwa na kiwanda kikubwa kitakachozalisha jozi 4,000 kwa siku”, alisisitiza Waziri Mhagama.

Kaimu Mkuu wa Kiwanda, Shalua Magandi alibainisha faida zinazotarajiwa kutokana na mradi wa kiwanda hicho ni pamoja na kutoa ajira 5,000 za moja kwa moja na zaidi ya ajira 4,000 kutokana na shughuli za uzalishaji nchini, kuongeza kodi kwa manispaa, bidhaa za ngozi zitakazouzwa ndani ya mkoa na mikoa jirani.

Ofisa masoko wa kiwanda hicho Fredrick Njoka aliwataka Watanzania kuendelea kununua viatu vinavyotengenezwa kwa ngozi kwa kuzingatia ubora na bei nafuu kwa kuwa kiwanda hicho kinatumia mashine za kisasa ambao ndiyo wenye ujuzi wa hali ya juu na teknoloji ya kisasa ya utengenezaji wa mashine hizo.

Kiwanda cha viatu cha gereza kuu Karanga, Moshi kilizinduliwa rasmi Juni 3, 1977 na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu, Julius Nyerere.Awali kilikuwa na ubia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF ambao baada ya mabadiliko ya kuunganishwa kwa mifuko hiyo , kwa sasa kina ubia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF.

Habari Kubwa