Magufuli asikia kilio cha wafanyabiashara

07Apr 2017
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Magufuli asikia kilio cha wafanyabiashara

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, (TPSF), Godfrey Simbeye, amesema Rais John Magufuli amesikia kilio cha wafanyabiashara kuhusu hali mbaya ya mazingira ya biashara na kuwaagiza mawaziri wake wawili kukaa pamoja na sekta binafsi ili kujadili changamoto zinazowakabili.

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, (TPSF), Godfrey Simbeye.

Simbeye alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa, hali ya biashara ni mbaya na imefikia hatua wafanyabiashara wamekata tamaa ya kufanya biashara.

Alisema hatua iliyofikia imewafanya wafanyabiashara kuiona serikali kama inataka kufanya biashara yenyewe.
Aidha, alisema baada ya malalamiko yao kumfikia Rais Magufuli, amewaagiza mawaziri wake wawili, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kukutana na sekta binafsi ili kujadili changamoto za sekta binafsi ziweze kufanyiwa kazi.

Alisema mkutano huo baina ya serikali na sekta binafsi unatarajiwa kufanyika Dodoma Jumanne ijayo.

“Mazingira ya biashara kwa sasa sio mazuri na baada ya malalamiko yetu ya mara kwa mara, Rais Magufuli amesikia na amemwagiza Mwijage na Waziri Mpango wakutane na sisi Dodoma kujadili changamoto zetu na mazingira ya biashara ambayo yamefanya wafanyabiashara kukosa kujiamini, hawana kwa sasa,

“Wafanyabiashara wanaona kama serikali haiwaamini, tunataka kujua tumekosea wapi, mpaka tunaona sasa serikali inataka kufanya biashara yenyewe kwa yenyewe. Tunataka kwenda kuyasema haya maneno Dodoma kupitia mkutano huo,” alisema Simbeye.

Habari Kubwa