Magunia yakwamisha korosho kwenda minadani

02Dec 2019
Hamisi Nasiri
MASASI
Nipashe
Magunia yakwamisha korosho kwenda minadani

SERIKALI imeombwa kuingilia kati suala la tatizo la ukosefu wa magunia ya kuhifadhia korosho za wakulima wilayani Masasi mkoani Mtwara.

magunia ya korosho.

Korosho nyingi za wakulima bado zipo majumbani, na zinashindwa kupelekwa katika minada kutokana na tatizo hilo.

Hayo yalisemwa na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kwenye kikao chao kwamba korosho nyingi bado zipo majumbani kwa wakulima, na zimehifadhiwa sakafuni na kwamba zinashindwa kukusanywa na kupelekwa katika minada inayofanyika kutokana na uhaba wa magunia.

Walisema hata idadi ya korosho zilizouzwa kwenye minada na zilizopo kwa wakulima kwa kukosa magunia idadi kubwa zile ambazo zimekwama kwa kukosa magunia ya kuhifadhia.

Musa Msanga, Diwani wa Lulindi, alisema wanaiomba serikali kuingilia kati suala la uhaba wa magunia.

Alisema korosho bado zipo kwa wakulima na wengi wanashindwa kupeleka korosho zao katika minada kwa sababu hawana magunia.

Naye diwani wa Lupaso alisema tatizo hilo la uhaba wa magunia katika chama kikuu cha wakulima Masasi-Masasi (MAMCU) zinaweza kufanya korosho nyingi za wakulima zikabaki bila ya kuuzwa na minada ikawa imefungwa.

Alisema serikali ichukuwe hatua za masukudi kuingilia kati na kutafutia ufumbuzi tatizo hili  ambalo limekuwa kero kwa wakulima.

Naye Diwani wa Nangoo, Mohammed Chilumba, alisema kila mwaka tatizo la uhaba wa magunia limekuwa likijitokeza, hivyo kufanya korosho nyingi kushindwa kuingia katika minada mpaka minada inafungwa korosho inakuwa bado zipo kwa wakulima bila kuuzwa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi, Juma Satma, alisema inashangaza kuona kila mwaka kunakuwa na tatizo la uhaba wa magunia.

  Alisema mkulima mtaji wake ni korosho hivyo anavyoshindwa kuuza korosho zake kwa sababu ya uhaba wa vifungashio vya kuhifadhia  korosho zao inashangaza.

"Tunaiomba serikali hasa wizara husika kuingilia kati tatizo hili la magunia kwani wakulima wengi korosho wameziweka majumbani kwao baada ya kukosa magunia ya kuwekea," alisema Satma. 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Alfred Francis, alisema alithibitisha kuwa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima Mtwara-Masasi (MAMCU) kina uhaba wa magunia.

Hata hivyo, Francis alisema tatizo hili bado wanalishughulikia na litakwisha siku chache zijazo.

Habari Kubwa