Mahakama yafuata wachafuzi pamba

09Aug 2016
Anceth Nyahore
Simiyu
Nipashe
Mahakama yafuata wachafuzi pamba

KATIKA moja ya mkakati wa kudhibiti uchafuzi wa zao la pamba mkoani Simiyu unaofanywa na wakulima na wanunuzi wasio waaminifu, Bodi ya Pamba (TCB) imekuja na mahakama zinazotembea kuwasaka wachafuzi hao katika wilaya ya Maswa mkoani humu.

Bodi hiyo imeamua kuwasaka na kuwachukulia hatua za kisheria wachafuzi wa pamba kwa kutumia mahakama inayotembea kwa sababu kitendo hicho kinaharibu soko la zao hilo kwa Tanzania, katika soko la dunia.

Akizungumza na Nipashe juzi wakati mahakama hiyo ilipoanza kutembelea vituo vinavyonunua zao hilo katika wilaya hiyo, Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Maswa, Ally Mabrouk alisema kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanunuzi wa zao hilo wanaokutwa na pamba chafu.

Umuazi huo umeungwa mkono na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka ambaye anasema utanusuru thamani na ubora wa zao kuu la biashara mkoani
humu.

Aidha, Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Maswa Mabrouk alisema baadhi ya kampuni zinazonunua zao hilo zina mtindo wa kuchezea mizani kwa lengo la kuwaibia wakulima.

Lakini, akasema zaidi Mabrouk, wakulima nao huongeza uzito kwenye pamba zao kwa kuweka maji na
mchanga.

“Zao la pamba linapoteza thamani kila kukicha huku mnunuzi akichezea mzani ili kumuibia mkulima na mkulima naye akitumia njia ya kuweka maji na mchanga," alisema Mabrouk.

"Na hayo yote ndiyo yanayolifanya zao hilo ambalo lilikuwa mkombozi wa wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa na kufikia kuitwa dhahabu nyeupe, kupoteza thamani yake.”

Mkaguzi huyo alisema wameamua kutumia mahakama hiyo ili kusikiliza na kutoa hukumu kwa watu wote ambao watakutwa wamefanya makosa ili kulinusuru zao hilo kupotea katika siku za usoni.

“Atakayekutwa na makosa wakati tunafanya ukaguzi wa zao la pamba katika maghala ya kununulia, hapohapo tunaanza kesi dhidi ya mtuhumiwa kwa kuwa mahakama hiyo ina hakimu, karani wa mahakama na askari polisi," alisema Mabrouk.
"Na ukipatikana na hatia unatumikia adhabu

Baadhi ya wanunuzi waliozungumza na Nipashe walisema hatua iliyochukuliwa na bodi hiyo ni nzuri, lakini imechelewa kuanza kutekelezwa kwasababu pamba imekuwa ikipata bei ya chini katika soko la dunia.

Mkuu wa Mkoa Mtaka alisema zoezi hilo ni mkakati wa mkoa wa kulinusuru zao la pamba.

“Zao la pamba hatuwezi kulinusuru kwa kutoa matamko kila siku na kukaa kwenye vikao na kulipana posho," alisema Mataka. "Ni lazima tutekeleze kwa vitendo."

"Kama Bodi ya Pamba ilivyoanza katika wilaya ya Maswa, ni vizuri na wakaguzi wengine wa wilaya za mkoa huo wakaanza zoezi hilo kwa kuwa lipo kisheria
na si geni.”