Mahenge aagiza wananchi wapewa maeneo mapya

16Mar 2019
Augusta Njoji
Chemba
Nipashe
Mahenge aagiza wananchi wapewa maeneo mapya

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Chemba kutenga maeneo mbadala na kuwapatia wananchi wa vijiji vya Bubutole na Mombose ambao watapisha ujenzi wa mradi wa bwawa la Farkwa.

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, picha mtandao

Dk. Mahenge alitoa agizo hilo jana, baada ya kutembelea vijiji hivyo vinavyotakiwa kupisha mradi huo.

Mkuu huyo aliutaka uongozi wa wilaya hiyo kuwahamisha mapema wananchi hao ili waweze kufanya shughuli za maendeleo.

“Serikali imehamia Dodoma, inahitaji maji ya kutosha na uthamini uliofanyika na jiji tayari umetumia zaidi ya Sh.milioni 200, kwa hiyo haiwezekani serikali kutumia fedha kurudi nyuma, huu mradi upo ni wajibu wako mkuu wa wilaya na timu yako kutekeleza hilo mapema,” alisema.

Aidha, alisema kwa sasa serikali inaendelea na mchakato wa kuandaa fidia za wananchi hao.

Awali, wananchi hao walimweleza mkuu huyo kuwa waliupokea mradi huo na kufanyiwa tathmini lakini hadi sasa hakuna mwananchi anayejua amefanyiwa tathmini anatakiwa kulipwa fidia kiasi gani hususan kwenye mashamba.

“Tathmini imefanyika mtu mwenye nyumba ndio anaweza kujua, lakini watu wenye mashamba mpaka sasa hatujui,” alisema mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Husna.

Alisema wananchi walikaa muda mrefu bila kujua hatima yao na kushindwa kuendeleza makazi yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, Dk. Semistatus Mashimba, alisema mwaka ujao wa fedha zimetengwa shilingi milioni 50 kwa ajili ya kupima maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya wananchi hao wanaohamishwa.

Aidha, alisema wamewasiliana na Wizara ya Maji ili kushirikiana nao kuhakikisha wananchi wanahamishwa salama na mali zao.

Habari Kubwa