Mahenge atoa somo kwa TRA ukusanyaji kodi

14Jan 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mahenge atoa somo kwa TRA ukusanyaji kodi

MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA), imetakiwa kuboresha uhusiano na wananchi na kubuni njia mpya za ukusanyaji mapato ili kuongeza kiwango cha mapato.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, picha na mtandao

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, alipokuwa akizindua jukwaa la wadau wa kodi mkoani humo.

Jukwaa hilo linalenga kubuni njia mpya za ukusanyaji wa mapato kwa kutoa elimu ya wafanyabiashara kuzingatia kulipa kodi.

Dk. Mahenge ambaye pia ni Mwenyekiti wa jukwaa hilo, alisema kuna kazi kubwa ya kufanya marejesho na kupendekeza mabadiliko katika sheria za kodi na kanuni zake.

"Pia kubuni njia ya kuzuia ukwepaji wa kodi tunawategemea mtusaidie moja ya eneo ni mahusiano kati ya TRA na wananchi," alisema.

Alieleza kuwa kama uhusiano huo utaboreshwa na kila mmoja akajua ni wajibu wake kulipa kodi, itawezesha ukusanyaji mzuri wa mapato.

"Ni wajibu wa kila mmoja na kutambua kuwa hawa hawakusanyi kuweka mifukoni mwao ni kwa ajili maendeleo naamini tutafanya vizuri," alisema.

Hata hivyo, alisema kuna baadhi ya watendaji wa TRA wanatumia lugha chafu kwa wateja na hawazingatii maadili yao ya kitaalamu.

Alisema wamekuwa wakikwaza wafanyabiashara na wawekezaji na kuanza kusema uongo kwenye mapato.

Naye, Meneja wa TRA mkoani humo, Kabula Mwemezi, alisema wamekuwa wakipata shida kuwatambua wanaofanya biashara bila kuwa na namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN).

"Mtu anafanya biashara vizuri, lakini hana TIN tunatafuta tufanyaje ili kuwatambua na tutumie mbinu gani tuweze kufanikiwa," alisema.

Hata hivyo, alisema kuna mwamko mdogo wa utayari wa kulipa kodi na kwamba kama kikiinuliwa itakuwa vyema.