Maisha nje ya mpunga yatajwa

14Nov 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Maisha nje ya mpunga yatajwa

WAKAZI wa Wilaya Malinyi mkoani Morogoro wametakiwa kuanza kufufua mazao ya biashara ya pamba na korosho badala ya kutegemea mpunga pekee kujiingizia kipato.

Mkuu wa wilaya hiyo, Majura Kasika ndiye aliyetoa wito huo juzi wakati akihutubia kwenye mkutano wa ufunguzi wa msimu mpya wa kilimo pamoja na kusikiliza kero za wakazi wake.

Alisema mazao ya pamba na korosho yalikoma kulimwa miaka 20 iliyopita kwa sababu ya uendashaji mbovu wa vyama vya ushirika uliosababisha wakulima kukopwa na kutolipwa kwa wakati.

"Sisi kama serikali tumeanza kuhamasisha ufufuaji wa kilimo cha mazao ya pamba na korosho, mazao ya biashara ambayo yalikuwa yakilimwa kwa wingi miaka ishirini iliyopita, hivyo ungeni mkono juhudi hizi," alisema Majura.

Alisema anajua kuwa waliamua kulima mpunga katika pori tengefu, maeneo oevu na hata kwenye hifadhi ya Bonde la Mto Kilombero baada ya uendeshaji huo mbovu wa vyama vya ushirika, lakini sasa hawana budi kurudi kwenye mazao ya biashara.

Mkuu huyo wa wilaya aliwaambia wakazi hao kuwa serikali imeanza jitihada za kuhifadhi bonde la mto huo ambalo kwa sehemu kubwa ndilo linalotoa maji ya Mto Rufiji, na ndiko kwenye mradi wa kuzalisha umeme Stiegler's Gorge utakaozalisha megawati 2,100 ukikamilika.

"Kutokana na hali hii, tumeanza kuwahamasisheni ufufuaji wa mazao makubwa yaliyowahi kulimwa miaka mingi iliyopita ya pamba na korosho, mazao haya yalionyesha ubora wa hali ya juu na hasa pamba ya Malinyi iliyosifika kwa kuwa nyeupe na nyuzi ndefu," alisema.

Majura aliwataka pia wakulima kutotegemea mazao ya chakula kama ya biashara kwa madai kwamba serikali inapodhibiti mfumuko wa bei za vyakula hujikuta wakiathirika.

Hivyo kila kaya ipande ekari moja ya zao la korosho, alisena na kuagiza shule za msingi na sekondari kupanda ekari tano za zao hilo kila moja.

Alisema kuwa ili kufanikisha mkakati wa kilimo cha mazao ya biashara, ameshamuagiza Afisa Kilimo wa wilaya hiyo, Martin Mhode kuanzisha mashamba na vitalu vya korosho na kwamba wilaya inategemea kupata miche 256,000 ya zao hilo.

Alifafanu kuwa miche hiyo itatolewa na Bodi ya Korosho na itagawiwa bure kwa wakulima.

Habari Kubwa