Maisha wachimbaji madini hatarini matumizi zebaki

14Feb 2020
Marco Maduhu
Geita
Nipashe
Maisha wachimbaji madini hatarini matumizi zebaki

MAISHA ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu nchini yapo hatarini kutokana na kutumika zebaki kuchenjulia dhahabu, bila ya kuvaa vifaa kinga.

Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Mtalingi Mine, uliopo Nyakagwe wilayani Geita, mkoani Geita, wakichenjua dhahabu kwa kutumia zebaki bila ya kuvaa vifaa kinga. PICHA: MARCO MADUHU

Hayo yalibainishwa juzi na Mkurugenzi wa Taasisi ya kiraia FADeV inayojishughulisha na kuendeleza wachimbaji wadogo wa madini nchini, Theonestina Mwasha, wakati alipoambatana na waandishi wa habari kwenye mgodi mdogo wa madini wa Mtalingi Mine uliopo eneo la Nyakagwe, wilayani Geita mkoani humo.

Mwasha alisema moja ya kazi wanayoifanya ya kuendeleza wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu, ni kutoa elimu ya usalama wao hasa wanapoingia chini ya maduara kuchimba dhahabu, pamoja na kutumia zebaki kuchenjulia dhahabu wavae vifaa kinga ili wawe salama na kuepuka athari mbalimbali.

“Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu idadi yao kubwa hawana elimu ya umuhimu kuvaa vifaa kinga pale wanapotafuta dhahabu wakiwa ndani ya maduara na hata kuchenjua dhahabu kwa kutumia zebaki, hawavai viatu vya usalama, groves, na kutumia mikono ikiwa tupu hali ambayo ni hatari kwa afya zao,” alisema Mwasha.

“Mchimbaji anavyo chenjua dhahabu mikono yake ikiwa tupu, akipatwa na mchubuko na zebaki ikiingia mwilini tayari inaanza kumletea madhara ya kiafya taratibu ikiwamo kichwa kuuma, kupoteza kumbukumbu, kutosikia, kuathiri figo na hatimaye kupoteza maisha,” aliongeza.

Mmoja wa wachimbaji hao, Boniphace Charles, alisema wanatambua kuwa zebaki ina madhara kwao na kubainisha kuwa walishazoea kuchenjua dhahabu wakiwa mikono peku, huku wakiomba elimu itolewe zaidi ya umuhimu wa kuvaa vifaa hivyo.

Naye mmiliki wa mgodi huo mdogo wa madini ya dhahabu, Mtalingi Hamzeh, alisema wanatambua madhara ya kutumia zebaki kuchenjulia dhahabu na kufafanua wanapogawa vifaa kinga kwa watumishi wao, hawavitumii licha ya awali kupewa elimu na taasisi hiyo ya FADeV, wakidai wameshazoea kufanya kazi wakiwa mikono tupu.

Alisema licha ya kutambua madhara hayo ya zebaki, na wachimbaji wadogo kutokuwa na mitaji mikubwa wameshindwa kumudu gharama za kutumia njia nyingine salama ya kuchenjulia dhahabu, na kutoa wito kwa taasisi za kifedha zitoe mikopo kwao ili waondokane na matumizi hayo ya zebaki.

Habari Kubwa