Majaliwa aipigia chapuo Vietnam kununua korosho

04Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majaliwa aipigia chapuo Vietnam kununua korosho

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, amewakaribisha wafanyabiashara kutoka nchini humo kununua korosho nchini ambazo amesema zipo za kutosha.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Balozi wa Vietnam hapa nchini, Nguyen Doanh, ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni, jijini Dar es Salaam, jana. PICHA: OWM

Pia amewataka wenye uwezo kutoka nchini humo, kujenga viwanda vya kuchakata korosho na kuahidi kuwa serikali iko tayari wakati wowote kuwasaidia pamoja na uwekezaji katika sekta zingine ikiwamo ya viwanda.

Majaliwa aliyasema hayo jana alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Vitemam nchini,  Balozi Nguyen Doanhm, ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam. 

Waziri Mkuu alisema Rais John Magufuli ameanzisha Wizara ya Uwekezaji iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kuifanya Tanzania kuwa mahali bora na salama kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Alisema ununuzi wa mazao ya kilimo kama vile pamba, korosho, kahawa na tumbaku ni fursa nyingine ya kibiashara ambayo wafanyabiashara wa Vietnam wanakaribishwa kuichangamkia.

Pia alitumia fursa hiyo kuwaalika wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Vietnam kuwekeza katika sekta ya viwanda hususani vile vinavyotumia malighafi za mazao ya kilimo zinazopatikana nchini na kwamba hatua hiyo itawawezesha wakulima wa Tanzania kuwa na soko la uhakika la mazao yao. 

"Serikali imeendelea kuondoa  vikwazo vya  kuanzisha na kuendesha  biashara kwa  kupitia upya   sheria, kanuni na taratibu za biashara  na kuzifuta zile  ambazo zimethibitika  kuwa zinayafanya mazingira ya biashara na uwekezaji kuwa magumu," alisema.

Kwa kuwa Vietnam imepiga hatua kubwa katika ujenzi na uendeshaji wa viwanda vya nguo, alisema Tanzania ingefurahi kuona viwanda vya aina hiyo vinajengwa nchini na wawekezaji kutoka nchi hiyo.

Kwa upande wake, Balozi Doanh alimweleza Waziri Mkuu juu wa ujio wa Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam,  Trinh Dinh Dung, anayetarajiwa kufanya ziara yake ya kikazi nchini kuanzia Julai 9 hadi 11, mwaka huu. 

Alisema Naibu Waziri Mkuu huyo anatarajiwa kuambatana na wafanyabiashara wasiopungua 20 kutoka kampuni kubwa za Vietnam.

Nchi za Vietnam na Tanzania zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1965 na mwaka 1984, Vietnam ilifungua ofisi ya ubalozi  wake hapa nchini kwa muda na kuufungua upya mwaka 2003.

Habari Kubwa