Majaliwa ataka matamasha kukuza biashara 

12Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majaliwa ataka matamasha kukuza biashara 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameitaka Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko ya Zanzibar kuhakikisha inatumia Tamasha la Biashara la Zanzibar kama chachu ya kukuza biashara ya Utalii kama ilivyo kwa Dubai Shooping Festival na matamasha mengine duniani.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiangalia asali iliyosindikwa na Kikosi cha Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU), wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Nne la Biashara la Zanzibar kwenye viwanja vya Maisara Mkoa wa Mjini Magharibi juzi. PICHA: OWM

“Natambua kwamba kazi ya kulipandisha hadhi zaidi tamasha letu hili si ndogo, hata hivyo ninayo imani kubwa kwamba  si tu uwezo wa kufikia malengo hayo mnayo bali pia mnaweza,” aliyasema hayo juzi jioni wakati akifungua Tamasha la Nne la Biashara la Zanzibar lililofanyika katika Wilaya ya Mjini  Mkoa wa Mjini Magharib. Tamasha hilo ni miongoni mwa shughuli mbalimbali za sherehe za maadhimisho ya  miaka 54 ya Mapinduzi  ya Zanzibar, ambazo zinafikia kilele  chake leo. Alisema Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko inatakiwa kutumia fursa ya uwapo wa tamasha hilo katika kuhakikisha inakuza biashara ya utalii kwa kuwa linajumuisha wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali. Waziri Mkuu alisema tamasha la biashara ni nyenzo muhimu ya kukuza biashara na huduma pamoja na kukuza uchumi wa nchi, pia linatoa fursa ya kuwakutanisha wafanyabiashara au watoa huduma na wateja wao. ”Hali hii humuwezesha mzalishaji kupata mrejesho kuhusu namna bidhaa yake inavyokubalika kwenye soko, mapungufu yaliyopo kwenye bidhaa husika pamoja na kuelewa maboresho anayotakiwa kuyafanya katika bidhaa au huduma.”

Alisema tamasha hilo linaweza kutumika kama nyenzo muhimu katika kuanzisha mahusiano mazuri ya kibiashara kati ya mteja  na mfanyabiashara, hivyo kuwawezesha wajasiriamali kuwa na masoko ya uhakika.

Baada ya ufunguzi, Majaliwa alitembelea mabanda mbalimbali yakiwemo ya taasisi za umma pamoja na wajasiriamali ambao wanatoka Zanzibar, Tanzania Bara, Kenya, Uturuki, Misri, Uganda na Burundi.

 Awali, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali, alisema tamasha hilo lenye washiriki zaidi ya 200 limeandaliwa na wizara yake pamoja na TanTrade.

 Balozi Amina alisema kauli mbiu ya tamasha hilo kwa mwaka 2018 ni ‘wekeza kwenye viwanda kwa uchumi na ajira’ inalengo la kuhamasisha wadau kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya falsafa na dhima ya ujenzi wa viwanda. 

Habari Kubwa