Majaliwa ataka Tanganyika Packers ianze uzalishaji

09Aug 2016
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Majaliwa ataka Tanganyika Packers ianze uzalishaji

WAZIRI Mkuu, Kassimu Majaliwa, ameiagiza Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kukamilisha haraka mikataba na mwekezaji wa kiwanda cha kusindika nyama cha Tanganyika Packers kilichopo mkoani Mbeya ili kianze kufanya kazi mapema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, na mkewe Mary, wakifurahia ngoma, baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Songwe.

Majaliwa alitoa agizo hilo juzi jioni katika ukumbi wa Ikulu ndogo mkoani Mbeya, baada ya kupokea taarifa ya Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla, iliyoeleza kuwa kiwanda hicho kilijengwa na kuwekwa mitambo tangu mwaka 1975, lakini hakijawahi kufanya kazi.

Makalla alieleza kuwa kwa sasa kiwanda hicho ambacho usimamizi wake upo chini ya Hazina kimeshapata mwekezaji, lakini akaiomba Serikali kuharakisha taratibu za mikataba ili kianze uzalishaji.

Alisema kuanza kufanya kazi kwa kiwanda hicho kutasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Mkoa wa Mbeya na kuwasaidia wafugaji thamani ya mifugo yao kuongezeka.

“Mkoa wa Mbeya una jumla ya viwanda 1,653 kati ya hivyo vikubwa ni tisa pekee, vya kati 19 na vidogo 1,625, Mkoa unazisimamia Halmashauri kutenga maeneo mengi zaidi ili kuongeza na kupanua viwanda vitakavyowezesha kukua kwa ajira kwa vijana,” alisema.

“Katika eneo hili tuna kiwanda cha kusindika nyama cha Tanganyika Packers, ambacho tangu kilipojengwa na kufungwa mitambo mwaka 1975, hakijawahi kufanya kazi, hivyo Serikali imefanya jitihada za kutafuta mwekezaji na amepatikana na kilichobaki ni kukamilisha mikataba ili kuanza kazi, mkoa unaiomba Serikali kuharakisha taratibu za mikataba ili kiwanda kianze kufanya kazi,” alisema Makalla.

Baada ya taarifa hiyo, Waziri Mkuu alitoa agizo kwa Wizara kuharakisha taratibu za mkataba ili kiwanda hicho kianze kufanya kazi na kwamba ni muhimu kwa uchumi wa mkoa na mtu mmoja mmoja.

Alisema kikifunguliwa wafugaji wa Mkoa wa Mbeya watafuga kwa tija.

“Mkoa wa Mbeya una viwanda vingi na naipongeza Serikali ya mkoa kwa kuwa na mipango mizuri ya kupanua viwanda hivyo, lakini viwanda vingi vikubwa havifanyi kazi kwa muda mrefu, kwa vile katika taarifa yako Mkuu wa Mkoa umesema mwekezaji wa kiwanda cha nyama amepatikana na tunaelewa umuhimu wa kiwanda hicho, naiagiza Wizara kuharakisha mikataba mwekezaji aanze uzalishaji,” alisema Majaliwa.

Vilevile Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Mkoa kuwaelimisha wafugaji namna bora ya ufugaji ili wazalishe mifugo yenye ubora ambayo itapata soko katika kiwanda hicho.

Alisema utaratibu wa kusafirisha mifugo kutoka mikoa ya mbali sio mzuri kwa kuwa hupunguza thamani ya mifugo ikiwamo ngozi na hata nyama kutokuwa nzuri kwa sababu mifugo hiyo husafiri umbali mrefu.

Aliwataka baadhi ya wafugaji ambao wana tabia ya kuichora mifugo yao kuacha utaratibu huo kwa maelezo kuwa kitendo hicho kinaharibu soko la ngozi.