Majaliwa ataka TRA imara

09Aug 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majaliwa ataka TRA imara

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa imeitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuimarisha kitengo cha tathmini ili kuweka viwango halali ambavyo havitawagandamiza wafanyabiashara.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa.

Aidha, Majaliwa alitaka kuwepo uwazi kuhusu viwango stahili vya kodi ambavyo wafanyabiashara hao wanapaswa kulipa, taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema jana.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo juzi alipozungumza na viongozi wa mikoa ya Mbeya, Katavi, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Iringa na Njombe; mara baada ya kuwasili mkoani Mbeya kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya maonyesho ya nane nane kwa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika mkoani humo.

"TRA waendelee kukusanya mapato vizuri, ila kuna wakusanya kodi wanaotaka kuharibu mkakati wa Serikali," alisema Majaliwa.

Wakusanya kodi wanaotaka kuharibu mkakati huo, alisema Majaliwa wanafanya mambo ya hovyo kwa kuwaongezea wafanyabiashara viwango vikubwa vya kodi kuliko stahili wanavyotakiwa kulipa.

Utaratibu huo, alisema Majaliwa unafanya ulipaji kodi uwe "kama tatizo au adhabu kwao jambo ambalo si sahihi."
"Naagiza watendaji wa TRA wanaofanya hivyo wasakwe na wachukuliwe hatua."

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Idara ya Uhamiaji ijikite katika kudhibiti watumishi wasiokuwa waaminifu ambao wamekuwa wakichukua rushwa kutoka kwa wageni na kuwaingiza nchini bila ya kuwa na vibali maalumu.

"Ni lazima tuhakikishe hakuna uingiaji holela ndani ya nchi na hasa kwa wanaoingia bila vibali maalumu."

Habari Kubwa