Majaliwa: Pamba yote itakuwa imenunuliwa ifikapo Julai 30

16Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majaliwa: Pamba yote itakuwa imenunuliwa ifikapo Julai 30

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema hadi kufikia Julai 30, mwaka huu, pamba yote iliyoko katika mikoa mbalimbali nchini inayolima zao hilo itakuwa imeshanunuliwa na wakulima wote kulipwa fedha zao.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa.

Kauli hiyo ilitolewa jana, na Waziri Mkuu alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Mbutu na Mwabakima wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora.

Alisema serikali imeamua kuingilia kati suala la ununuzi wa zao la pamba kutokana na kusuasua kwa soko lake kwa kutoa dhamana ili kuwawezesha wanunuzi kukopeshwa fedha na benki mbalimbali kwa ajili ya kununulia pamba kutoka kwa wakulima.

Hivyo, aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya katika maeneo yote yanayolima zao hilo wawasimamie ipasavyo wanunuzi wote ili kuhakikisha fedha zitakazopatikana zinakwenda kutumika kwa ajili ya kununulia pamba na si vinginevyo, ambapo kibali cha dhamana kinatarajia kutoka leo.

Amesema kumekuwa na kusuasua kwa ununuzi wa zao hilo tangu kuanza kwa msimu wa mwaka huu, jambo ambalo serikali haiwezi kulifumbia macho suala hilo, hivyo jana alikutana na kufanya mazungumzo na wadau wa zao hilo wakiwamo wanunuzi na wamekubaliana kununua pamba yote.

“Tunatambua adha mliyoipata tangu kuanza kwa msimu wa mwaka huu na hayo ni mapito tu. Nawasihi muwe na amani kwani serikali yenu inafuatilia suala hili na Rais John Magufuli anataka kuona pamba yote inatoka kwa wakulima ili kuwawezesha kupata tija.”

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwasihi wakulima wa pamba na wakulima wa mazao mengine nchini wahakikishe mara baada ya kuuza mazao yao wanatenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kununulia pembejeo watakazozitumia katika msimu ujao.

Awali, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema serikali itahakikisha inaendelea kutafuta masoko ya mazao hayo ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha wakulima kuwa na uhakika wa masoko kwa mazao yao na hivyo kujiongezea tija.

Pia, waziri huyo amesema mbali na kutafuta masoko, serikali imedhamiria kufufua viwanda mbalimbali vya nguo hapa nchini ili kuwawezesha wakulima wa zao la pamba kuwa na soko la uhakika. “Kuhusu suala la maghala tunatambua tatizo hilo na tutahakikisha tunayaboresha ili pamba iweze kuhifadhiwa katika mazingira bora.”