Majitaka yawaondoa wapangaji wa NHC

21May 2020
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Majitaka yawaondoa wapangaji wa NHC

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya imelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuwaondoa wapangaji wote katika jengo la Cinema lililopo katikati ya Jiji.

Uamuzi huo umetokana na shirika  kushindwa kuweka miundombinu ya majitaka, hali inayosababisha maji machafu kutiririka ovyo mitaani na kuhatarisha afya za wananchi.

Jengo la cinema lenye ghorofa moja ambalo ni mali ya shirika hilo lipo mtaa wa Lupa, mkabala na Posta, katikati ya Jiji la Mbeya, lina wapangaji zaidi ya 15, lakini halina mfumo wa majitaka.

Akizungumza na Nipashe juzi, Ofisa Afya wa Kata ya Sisimba, John Oden, alisema aliamua kuchukua hatua ya kuwahamisha wapangaji hao kwa lengo la kunusuru afya zao.

Alisema uamuzi huo uko kwa mujibu wa sheria na kwamba anachokifanya sasa ni kuandika notisi ya kuwaondoa wapangaji wote hadi hapo atakaporekebisha mfumo wa majitaka.

Hata hivyo, baadhi ya watumiaji wa jengo hilo, walisema kukosekana kwa miundombinu ya majitaka imekuwa ni hatari kwao kutokana na harufu mbaya.

Mmoja wa wapangaji hao, Brighton Ngowi, alisema jengo hilo ambalo wanalitumia kibiashara, limekuwa likisababisha kero kwa wateja na wananchi wengine kutokana na hafuru inayosikika.

Akizungumzia kadhia hiyo, Meneja wa Shirika hilo Mkoa wa Mbeya, Said Bundala, alisema wameshachukua hatua kwa kulipia gharama za uwekaji wa mfumo wa majitaka katika jengo hilo.

Alisema zaidi kuwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mkoani humo, ndiyo inayosuasua kufanya kazi hiyo, huku mkuu wa kitengo cha mfumo wa majitaka wa mamlaka hiyo, Mhandisi Yasin Msuya, akieleza changamoto zinazokwamisha kazi hiyo kufanyika kuwa ni wananchi kuendeleza shughuli za ujenzi kwenye maeneo ambayo yanahitaji huduma za kijamii.

Habari Kubwa