Maktaba Z'bar yasaidiwa M10/-

14Feb 2016
Frank Monyo
Nipashe Jumapili
Maktaba Z'bar yasaidiwa M10/-

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Ufundi Zanzibar, Abdalla Mzee, amepokea msaada wa shilingi milioni 10 kwa ajili ya Maktaba Kuu uliotolewa na kampuni ya simu ya mkononi ya Zantel.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Mzee alisema fedha hizo zitasaidia katika kurahisisha upatikanaji wa vitabu na hivyo kuimarisha mazingira ya utoaji maarifa na kuendeleza elimu Zanzibar .

Alisema msaada huo utasaidia pia katika uboreshaji wa maktaba katika visiwa vya Zanzibar, hasa kuongeza wigo wa kupata taarifa kutoka mtandaoni.

“Kazi kubwa ya maktaba Zanzibar ni kuhakikisha inatoa huduma kwa lengo la kuongeza ujuzi na maarifa miongoni mwa Wazanzibar, na hivyo basi msaada huu kutoka Zantel utaleta msukumo wa utekelezaji wa azma yetu hiyo,” alisema.

Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Zantel, Benoit Janin alisema msaada huo kwa maktaba ya Zanzibar unalenga kukuza na kusaidia kurahisisha upatikanaji wa maarifa miongoni mwa jamii ya Wazanzibar.

Alisema maktaba ni njia pekee na rahisi ya kusaidia upatikanaji wa maarifa na kuongeza uelewa miongoni mwa wanajamii bila kujali tofauti zao za kiuchumi.

“Maktaba ya Zanzibar, ina jukumu la kuhakikisha inatoa huduma bora na zenye ufanisi zinazokidhi mahitaji ya wakazi wanaoishi mijini na vijijini kupata elimu, habari, kufahamu habari za utamaduni na burudani kwa usawa bila upendeleo;” alisema.

Alisisitiza kuwa kampuni yake inayoongoza Zanzibar, inaona fahari kushiriki katika kuchangia ukuaji na ustawi wa jamii katika sekta mbalimbali.

Habari Kubwa