Makumbusho yatakiwa kujiendesha kibiashara

11Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Makumbusho yatakiwa kujiendesha kibiashara

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, amelitaka Shirika la Makumbusho ya Taifa kujiendesha kibiashara badala ya kujikita kwenye kuhifadhi pekee.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, picha mtandao

Alitoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na watumishi wa shirika hilo wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Makumbusho hiyo jijini Dar es Salaam.

Alisema shirika hilo linatakiwa kuhifadhi kimkakati badala ya kujikita kutoa huduma kwa wananchi bila ya kuwa na mkakati madhubuti wa kukusanya mapato ambayo hayategemei fedha kutoka Serikali Kuu.

Alifafanua kuwa shirika hilo limekuwa dhoofu kimapato hivyo linatakiwa kuachana na mawazo ya kizamani kuwa jukumu lao ni kuhifadhi pekee badala yake ianze kufikiri itawezaje kuingiza mapato kama vile ilivyo kwa Shirika la Hifadhi za Taifa pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania.

''Nawaagiza fikirieni namna mtakavyoweza kutoa huduma kibiashara ili watalii kutoka nje waje hapa watoe hela,'' alisema Kanyasu.
Alisema shirika hilo linatakiwa kujitegemea kimapato tofauti na ilivyo sasa na limekuwa likitegemea kila kitu kutoka Serikali Kuu ilhali lina kila kitu cha kuweza kuwaingizia mapato.

Kanyasu alisema shirika hilo linatakiwa kuwaza kibiashara kwa kila kitu wanachohifadhi kwa vile shabaha ya serikali ya awamu ya tano kwa sasa ni kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii maradufu.

''Tunataka mfikie hatua ya kuanza kutoa gawio kwa serikali, lakini kama hamtabadilika mtajikuta kuna siku shirika hili linafutwa kwa vile ni mzigo kwa serikali,'' alisema Kanyasu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Mawazo Ramadhani, alisema agizo hilo litatekelezwa kwa kuanza kutilia mkazo suala la mapato yataokanayo na watalii.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi huyo alimweleza Naibu Waziri huyo kuwa tayari wameshaanza kubuni mikakati ya kuhakikisha shirika hilo linaimarika kimapato kwa kuanza kuhamasisha wanafunzi vyuoni.