Makusanyo majengo yaongezeka kwa 20%

14Sep 2017
Augusta Njoji
Nipashe
Makusanyo majengo yaongezeka kwa 20%

BUNGE limeelezwa kuwa makusanyo yanayotokana na kodi za majengo kutoka Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji 30 yaliyokuwa yakisimamiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) yameongezeka kwa asilimia 20.6.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji.

Hayo yalielezwa jana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Cecilia Paresso.

Paresso alitaka kujua baada ya TRA kupewa jukumu la kukusanya kodi hiyo ufanisi umefikiwa kwa kiasi gani ikilinganishwa na mapato yaliyokuwa yakikusanywa na halmashauri zenyewe.
 
“Kwa kuwa kodi ya majengo ilikuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji na majukumu ya kutoa huduma kwa wananchi hayajapunguzwa, je, serikali imejipanga vipi kufidia vyanzo hivyo vilivyopotea?”Alihoji Paresso.

Mbunge huyo alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 serikali ilitangaza kuzinyang’anya Halmashauri uwezo wa kukusanya mapato ya kodi ya majengo na kuagiza kodi hiyo kukusanywa na TRA.

Akijibu swali hilo, Dk. Kijaji alisema katika mwaka 2015/16 zilikusanywa na serikali za mitaa Sh. bilioni 28.28,  lakini zimeongezeka na kufikia Sh. bilioni 34.09 kwa mwaka 2016/17 kipindi ambacho TRA ilikusanya kodi hiyo.

“Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 20.6 ya makusanyo ya Halmashauri husika kabla ya kodi hiyo kuhamishiwa TRA,” alisema Dk. Kijaji.

Alieleza kuwa serikali inatambua kodi ya majengo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji katika kutekeleza mipango ya utoaji wa huduma za jamii.

Hata hivyo, alisema hatua ya serikali kuhamishia jukumu hilo la ukusanyaji wa kodi ya majengo TRA haikulenga kuzinyang’anya Halmashauri vyanzo vya mapato bali kuimarisha ukusanyaji wake.

Alisema takwimu zinadhihirisha kuwa TRA imefanya vema katika kukusanya mapato hayo ikilinganishwa na Halmashauri.

Dk. Kijaji alisema serikali imeweka utaratibu wa kibajeti ambao unaziwezesha Halmashauri kupata fedha za makusanyo ya kodi ya majengo iliyokusanywa na TRA, ili kuziwezesha kutimiza majukumu yao.

Alisema utaratibu uliopo Halmashauri zinatakiwa kuomba fedha hizo kutoka Serikali Kuu kwa kuzingatia makisio ya bajeti zao.
000000
Tatizo sugu maji lakumba gereza
SERIKALI imekiri kuwapo kwa tatizo kubwa la upatikanaji wa maji katika Gereza la Kibondo mkoani Kigoma.

Aliyethibitisha tatizo hilo ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, alipokuwa akijibu swali la Mbunge Muhambwe (CCM), Atashasta Nditiye, ambaye alitaka kujua ni lini serikali itamaliza tatizo la maji katika gereza hilo na wakati unaofaa, ili kupeleka mradi mkubwa wa maji kwenye gereza utakaolinda afya za askari walioko gerezani na watu wengine.

Akijibu swali hilo, Masauni alisema katika mwaka 2010 serikali ilianza mchakato wa kumaliza tatizo hilo kwa kutenga bajeti ya Sh. milioni 20 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu na kazi hiyo ilifanywa na Wakala wa Uchimbaji Mabwawa na Visima (DDCA) iliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam.

Masauni alisema uchimbaji wa kisima katika gereza hilo ulikamilika Oktoba 2, 2010 na kilikuwa na uwezo wa kutoa lita 2300 kwa saa ambazo ni sawa na lita 55,200 kwa siku.

“Kiasi hiki ni kidogo sana ukilinganisha na mahitaji ya maji gerezani ambayo ni lita 94,870 kwa siku, hivyo kubakiwa na upungufu wa lita 39,670 kwa siku,” alisema Masauni.

Naibu Waziri alisema mwaka 2014 upembuzi yakinifu ulifanywa na wataalamu wa Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na mhandisi wa Mamlaka ya Maji Wilaya ya Kibondo na kushauri kuwa gereza hilo liondokane na tatizo la maji ambapo magereza wanatakiwa kuvuta maji kutoka mtandao wa halmashauri kwa gharama ya Sh. milioni  330.4.

Habari Kubwa