Makusanyo ya kodi yadaiwa kukwamisha miradi ya mil. 700/-

20Dec 2016
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Makusanyo ya kodi yadaiwa kukwamisha miradi ya mil. 700/-

UAMUZI wa serikali wa kufanya mabadiliko yanayolenga kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kwa kukabidhi jukumu hilo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), umeanza kuiathiri Manispaa ya Moshi baada ya baadhi ya miradi yake inayofikia Sh. milioni 700 kukwama.

Meya wa Manispaa hiyo, Raymond Mboya, alisema miradi hiyo haitekelezeki, kwa kuwa fedha zilizokuwa zitumike, ambazo zilitengwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017, hazikukusanywa kutokana na jukumu hilo kuondolewa mikononi mwa halmashauri.

“Halmashauri ya Manispaa ya Moshi tulikusudia kukusanya zaidi ya Sh. bilioni 7.2, kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, lakini baadhi ya miradi imekwama kutokana na upungufu uliopo katika mpango wa bajeti,” alisema.

Alisema hatua ya serikali kuondoa kodi ya majengo iliyokuwa ikikusanywa na halmashauri hiyo na jukumu hilo kuhamishiwa TRA, kunaifanya ishindwe kutekeleza baadhi ya miradi yake.

Alisema bajeti ya halmashauri hiyo imeathirika kwa zaidi ya asilimia 16 na hivyo baadhi ya miradi haitatekelezeka, licha ya kuamua kupunguza ukubwa wa ujenzi wa miradi ya barabara ambayo baadhi ya makandarasi walikuwa kazini.

Alitoa mfano wa kodi mbalimbali ikiwamo ya majengo, zilipaswa kuanza kukusanywa na TRA kuanzia Julai mosi, mwaka huu baada ya uamuzi huo wa serikali.

Alisisitiza kukwama kwa baadhi ya miradi ya Manispaa ya Moshi kunaifanya ielekeze nguvu zake kuboresha bajeti yake ya mwaka 2017/18 ili kutekeleza miradi hiyo.

Aliiomba serikali kurejesha makusanyo ya kodi za nyumba kurudishwa halmashauri za miji na manispaa badala ya kukusanywa na TRA ili ziweze kujiendesha na kutekeleza miradi mbalimbali ya kuleta maendeleo ya wananchi.

Habari Kubwa