Malipo korosho yadodesha watoto kujiunga sekondari

13Jan 2019
Hamisi Nasiri
Masasi
Nipashe Jumapili
Malipo korosho yadodesha watoto kujiunga sekondari

 WANAFUNZI 53 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Kutwa Lupaso, Masasi mkoani Mtwara, hawajaripoti shuleni hadi sasa kutokana na wazazi na walezi wao kutolipwa fedha za korosho.

Kata ya Lupaso iko katika kijiji cha Lupaso ambacho Rais wa awamu tatu, Benjamin Mkapa, anakotoka na inazalisha korosho kwa kiasi kikubwa lakini msimu huu wakulima wengi waliouza korosho bado hawajalipwa fedha zao hadi sasa.  

Diwani wa Lupaso, Douglas Mkapa, alisema hayo alipofanya ziara kwenye shule hiyo kwa ajili ya kuangalia hali ya wanafunzi ambao wameteuliwa kujiunga na shule hiyo kama wamesharipoti baada ya shule kufunguliwa tangu Januari 7, mwaka huu.

Mkapa alisema baada ya kutembelea shule hiyo kujionea kama wanafunzi wameripoti, alielezea kusikitishwa kuona hadi sasa wanafunzi 53 ambao wamechaguliwa na kupangiwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza, hawajaripoti.

Alisema akiwa diwani wa kata hiyo, alishapata taarifa baada ya kukutana na wazazi na walezi hivi karibuni na kumweleza kuwa hali zao za kiuchumi kwa sasa si nzuri kwa sababu wengi wameuza korosho na hadi sasa hawajalipwa.

Mkapa aliongeza kuwa wazazi na walezi wengi wa kata ya Lupaso ni wakulima hasa wa korosho, hivyo kutokana na serikali kutowalipa fedha zao, watoto wao wameshindwa kuripoti shuleni kwa vile wazazi na walezi hawana fedha za kuwanunulia mahitaji ya msingi zikiwamo sare.

Kwa mujibu wa diwani huyo, hadi sasa wakulima ambao baadhi yao ni wazazi na walezi waliouzia korosho zao katika Chama cha Ushirika cha Lipumbulu, hakuna ambaye amelipwa fedha.

Alisema hali hiyo inasababisha wanafunzi wengi, wakiwemo wa shule za msingi kushindwa kuripoti shuleni hadi pale serikali itakapowalipa wakulima fedha zao.

“Kwa sasa hali ya uchumi ya wananchi wa kata yangu ni ngumu sana kwani wanashindwa hata kuandaa mashamba yao kwa vile hajalipwa fedha zao za korosho. Pia tatizo hili la wanafunzi kushindwa kuripoti shuleni hadi sasa pia linachangiwa na malipo ya korosho kuchulewa,” alisema Mkapa.

Abdul Abdul, mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao, alisema wao si kwamba hawataki watoto wao wasiende shuleni lakini kutokana na hali zao za kiuchumi kwa sasa ni ngumu kwa vile tegemeo lao kubwa la kupata fedha ni katika zao la korosho na tayari wameshauza lakini hadi sasa bado hawajalipwa fedha zao.

“Tunawapelekaje watoto wetu shuleni wakati hata hiyo serikali inajua kuwa sisi watu wa kusini tegemeo letu kubwa la uchumi ni  korosho na tumeshauza lakini fedha zetu bado hatujalipwa. Serikali itakapotulipa watakwenda shuleni kwa sababu tunapata fedha za kununua mahitaji,” alisema Abdul.

Mzazi mwingine, Dullah Alhamisi, alisema anaiomba serikali kuharakisha malipo ya korosho ili kila mzazi ambaye mtoto wake amepata nafasi ya kujiunga na masomo ya sekondari, amnunulie mahitaji ya msingi ya shule hatimaye mtoto aende shuleni.

Mkuu wa Shule hiyo, Pancras Ajali, alikiri kuwa wanafunzi hao 53 ambao 26 ni wasichana na 27 ni wavulana, bado hawajaripoti shuleni hadi sasa licha ya shule kufunguliwa tangu Januari 7.

Habari Kubwa