Malori ya magendo kutaifishwa

27Jun 2017
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Malori ya magendo kutaifishwa

SERIKALI imesema kuanzia sasa itataifisha mahindi na malori yote yatakayokamatwa yakivusha chakula kwa magendo kwenda nje ya nchi.

Hatua hiyo ilitangazwa jana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati akizungumza na maelfu ya waumini wa Kiislamu baada ya kumalizika kwa Swala na Baraza la Idd El Fitri kitaifa iliyofanyika katika Msikiti wa Riadha Moshi Mjini.

“Kuanzia leo mtu yeyote atakayekamatwa anasafirisha mahindi kwenda nje ya nchi, mahindi hayo tutayataifisha na tutayapeleka kwenye ghala la taifa la chakula na gari lake tutalitaifisha na litaishia Jeshi la Polisi," alisema Majaliwa.

"Tunayafanya haya kwa lengo la kuwalinda Watanzania wasikumbwe na njaa… natoa wito kwa wafanyabiashara kujiepusha na jambo hili ambalo linaweza kuwaletea hasara isiyokuwa muhimu.”

Waziri Mkuu alisema hadi kufikia jana, serikali ilikuwa imepokea maombi kutoka nchi za Somalia, Ethiopia, Sudani ya Kusini na JK Kongo zikitaka kupatiwa msaada wa chakula.

“Leo hii (jana), nchi hizo zilikuwa zimetuandikia barua rasmi wakiomba kupewa msaada wa chakula, wakati huo na sisi huku ndani hatuna chakula cha kutosha," alisema Majaliwa.

"Ni marufuku kwa yeyote kusafirisha chakula kwenda nje ya nchi bila ya vibali kwa sababu serikali imehamasisha kuwa na viwanda nchini na kama tutatoa vibali, basi chakula hicho tutaanza kukisaga ili upelekwe unga na siyo mahindi.”

Alisema wamegundua kuna maeneo ambayo hayakupata mvua vizuri msimu huu na uzalishaji wa chakula umekuwa mdogo katika maeneo hayo.

"Ndiyo maana serikali imeanza kuwahamasisha wafanyabiashara kuchukua chakula kwenye maeneo yaliyo na mavuno mengi na kupeleka maeneo yenye mavuno kidogo ili kusambaza chakula tulichokipata," alisema.

“Serikali haijaruhusu bado kutoa chakula kwenda nje ya nchi, (lakini) kumekuwa na wimbi kubwa la usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi bila vibali.
"Hilo ni kosa kubwa; kwa sababu hiyo tunapelekea nchi yetu kupata baa la njaa.”

Alieleza kusikitishwa na jinsi mipaka ya Tarakea, Holili, Mwanga, Horohoro, Siha, Namanga na Sirari iliyoko katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Mara inavyopitisha idadi kubwa ya chakula cha magendo kwenda nje ya nchi licha ya zuio.

“Kama kweli unaona kuna umuhimu wa kupeleka chakula nje, kwanza kaombe kibali na kitakuruhusu kusaga na kupeleka unga na siyo mahindi," alisema.

"Kwa kupeleka mahindi unapunguza ajira ya nchi kwenye viwanda vyetu, pili watu hutoa mahindi holela, tunashindwa kupata takwimu sahihi za uharibifu huo.”

Alisema kama ni biashara, Tarakea kuna soko, lakini hakuna sababu ya kupeleka malori zaidi ya 100 kwa sababu ni kata yenye watu wasiozidi 4,000.

Juzi, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu alikamata magunia 1,639 sawa na tani 164 katika eneo la West Kilimanjaro yakisafirishwa kwa magendo na wafanyabiashara kwenda nchi za Kenya, Ethiopia, Somalia na Sudani ya Kusini ambazo zinakabiliwa na njaa.

Kutokana na hali ya chakula inayoonekana, Waziri Mkuu aliwataka wafanyabiashara wa mahindi kuuza mazao hayo katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza na Geita ambayo amedai wananchi wanahitaji chakula hicho.

Habari Kubwa